Kamanda wa waasi akamatwa Ufilipino

Maafisa wa usalama wa Ufilipino wamesema wamemtia mbaroni kamanda mmoja wa waasi, muda mfupi baada ya muda wa kusimamisha mapambano msimu wa Krismasi kukamilika.

Image caption Polisi Manila Ufilipino

Tirso Alcantara, anayejulikana pia kwa jina la Comrade Bart, alijeruhiwa alipojaribu kuchomoa bastola baada ya kuvamiwa na kikosi maalumu cha jeshi, katika kijiji kimoja Kusini mwa Mji Mkuu wa Manila, baada ya kusalitiwa na raia.

Mwandishi wa BBC mjini Manila, anasema kukamatwa kwa kamanda huyo ni faraja kubwa kwa jeshi, lakini kutavuruga mashauriano ya amani.

Serikali ya Rais Benigno Aquino, imekubali kufanya mashauriano na waasi mwezi ujao nchini Norway.

Hizo ni juhudi za Serikali za kumaliza uasi wa kikomunisti ulioendelea nchini humo kwa zaidi ya miaka 42 na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.