Wenger aridhishwa ukomavu wa wachezaji

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amesema amefurahishwa na ukomavu wa mawazo na nguvu wa wachezaji wake, baada ya kuhimili mechi ngumu dhidi ya Birmingham na kushinda 3-0.

Image caption Arsene Wenger

Mabao ya Robin van Persie, Samir Nasri na la kujifunga la mlinzi wa Birmingham, Roger Johnson, yaliipatia ushindi mnono Arsenal na kuzidi kuwaweka katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya soka ya England.

Baada ya mchezo huo ulioshuhudia rafu kadha mbaya, Wenger amesema: "Tulikabiliana vizuri na kila kitu tulichokuwa tukitendewa."

"Rafu mbaya tulizochezewa - tuliweza kuwa watulivu na kuendelea kucheza soka yetu."

Wenger aliiambia BBC: "Tulikuwa na mechi ngumu. Timu ilionekana kuwa imara sana na itaendelea kuimarika kadri siku zinavyokwenda."

Mlinzi wa Birmingham Johnson, alioneshwa kadi ya manjano mapema kipindi cha kwanza baada ya kumchezea rafu mbaya Cesc Fabregas, na Lee Bowyer alionekana kumkanyaga kwa makusudi Bacary Sagna.

Mwezi wa Februari mwaka 2008, timu hizi mbili zilitupiana maneno baada ya Martin Taylor wa Birmingham kumchezea rafu mbaya mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Eduardo na kumvunja mguu.

Ushindi dhidi ya Birmingham katika uwanja wa St Andrew safari hii, ni ushahidi tosha kwamba Arsenal inajifunza namna ya kushinda katika mazingira magumu na uwanja ambao wapinzani wake wanaowania ubingwa wamepoteza pointi.

Chelsea ilipoteza mechi yake dhidi ya Birmingham mwezi wa Novemba, wakati Manchester United ilitoka sare na timu hiyo siku ya Jumanne iliyopita.