Tamko halijatolewa kuhusu Avram Grant

Timu inayoburura mkia katika msimamo wa Ligi Kuu ya soka ya England, West Ham, imesisitiza hakuna tangazo litakalotolewa kuhusiana na mustakabali wa meneja wao anayekabiliwa na changizo kubwa, Avram Grant.

Image caption Avram Grant

BBC kupitia kitengo chake cha michezo, kimebaini, Martin O'Neill, anaandaliwa kuchukua nafasi ya Grant, raia wa Israel, aliyeshuhudia timu yake ikipoteza mchezo uwanja wa nyumbani wa Upton Park siku ya Jumamosi dhidi ya Arsenal.

Image caption Theo Walcott

Arsenal waliishindilia West Ham mabao 3-0 katika mechi hiyo na kuzidi kung'ang'ania nafasi yao na ya tatu, wakitia kibindoni pointi 43. mabao ya Arsenal yalipachikwa na Van Parsie mawili na Walcott.

Ilikuwa ni mechi ya pili tu kwa West Ham kupoteza katika michezo minane iliyopita, lakini Grant alionekana mwenye wasiwasi mwingi wakati akiondoka uwanjani.

Grant mwenye umri wa miaka 55, aliwapigia makofi na kuwapungia mashabiki, wakati akiondoka uwanjani na akawatupia skafu yake ya kuzuia baridi, kabla ya kupotea ndani ya vyumba vya wachezaji uwanja wa Upton Park.

O'Neill, mwenye umri wa miaka 58, aliondoka Aston Villa katika hali ya kutatanisha, wakati wa mkesha wa kuanza msimu huu.