Kesi ya daktari wa Michael Jackson

Dr Conrad Murray
Image caption Dr Conrad Murray

Jaji amemwamuru daktari binafsi wa Michael Jackson ashtakiwe kwa kuua bila kukusudia.

Jaji Michael Pastor alitoa uamuzi huo dhidi ya Dr Conard Murray katika kesi ya awali mjini Los Angeles.

Waendesha mashtaka walisema kwamba alimgawia dawa ya usingizi yenye sumu iliyochanganywa na dawa nyingine na kushindwa kumhudumia ipasavyo.

Dr Murray, mwenye umri wa miaka 57, amekana kuhusika na makosa hayo, na kusema hakumgawia Jackson chochote chenye sumu.

Jaji Pastor ametoa amri hiyo dhidi ya mtaalamu huyo wa moyo katika siku ya sita ya kesi hiyo.

Pia ameiomba bodi ya utabibu ya California kufuta leseni ya Dr Murray itakayomzuia kufanya kazi kwenye jimbo hilo.

Dr Murray anakabiliwa na kifungo cha miaka minne gerezani iwapo atapatikana na hatia.