Goodluck wa Nigeria apita mchujo

Rais Goodluck Jonathan
Image caption Rais Goodluck Jonathan

Rais Goodluck Jonathan amechaguliwa kugombea kiti cha urais kwa tiketi ya chama tawala katika uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika mwezi Aprili.

Aliyekuwa makamu wa Rais Atiku Abubakar ndiye aliyekuwa mpinzani mkuu wa Bw Jonathan ambaye aliungwa mkono na vigogo wenye ushawishi mkubwa katika sehemu za kaskazini mwa nchi hiyo.

Rais Jonathan alishinda kwenye uteuzi huo ingawaje baadhi ya wajumbe walisema chama hicho kilipaswa kuchagua mgombea mwingine.

Mgombea wa PDP ameshinda kila uchaguzi tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi mwaka 1999, kwa hiyo mgombea wake anatarajiwa kuungwa mkono zaidi.

PDP kina desturi ya kubadilishana uongozi baina ya kaskazini na kusini baada ya kukaa madarakani kwa mihula miwili lakini hii ilivurugwa baada ya Bw Jonathan, kutoka kusini, kumrithi Umaru Yar'Adua alipofariki mwaka jana.

Bw Jonathan kisha aliwania na kushinda ugavana wa jimbo lake Bayelsa baada ya aliyekuwa gavana kuondolewa mamlakani kwa tuhuma za ufisadi.

Image caption Bw Abubakar Atiku

Bw Jonathan alishinda kwa kura 2,736 huku Bw Abubakar akipata kura 805. Sarah Gibril alichukua nafasi ya tatu baada ya kupata kura moja.

Waandishi wanasema ushindi wa Rais Jonathan haukutarajiwa huku baadhi ya majimbo ya Kusini na Kaskazini mwa nchi hiyo wakimwuunga mkono.

Hata hivyo msemaji wa Bw Abubakar amelalamika kuwepo kwa udanganyifu.

Ingawaje baadhi walitazamia kuwa Abubakar angeondoka kwenye chama cha PDP iwapo angeshindwa, alimpongeza Jonathan kwa ushindi huo.