Mtu mmoja ajiteketeza mjini Cairo

Cairo
Image caption Cairo

Mtu mmoja alijiteketeza nje ya jengo la bunge katika mji mkuu wa Misri, Cairo.

Walioshuhudia walisema mtu huyo alijimwagia mafuta kwenye nguo zake kabla ya kujiwasha moto.

Moto huo ulizimwa na afisa wa polisi na mtu huyo alipelekwa hospitali- hali yake bado haijajulikana iko vipi.

Hatua hiyo imefanana na ile ya raia wa Tunisia mwenye umri wa miaka 26 ambapo hatua yake ya kujitoa kafara uliamsha maandamano nchini humo na kusababisha kuvunjika kwa serikali.

Mtu huyo wa Cairo mwenye umri wa miaka 49 ametambuliwa kuwa mmiliki wa mgahawa kutoka mji wa Ismailia, mashariki mwa mji mkuu.

Shirika la habari la Reuters limemnukuu shahidi mmoja akisema aliungua kwenye mikono na uso.

Nia yake haikuwa wazi lakini chanzo kutoka wizara ya mambo ya ndani imeiambia Reuters kwamba alifanya hivyo kupinga hali yake duni ya maisha.