Darren Bent kujiunga na Aston Villa

Mshambuliaji Darren Bent anakaribia kukamilisha uhamisho kutoka klabu ya Sunderland na kujiunga na Aston Villa.

Image caption Darren Bent

Ada ya paundi milioni 18 inaaminika imeafikiwa kwa ajili ya mshambuliaji huyo anayechezea pia timu ya taifa ya England, baada ya Bent kuwasilisha barua ya maombi ya uhamisho.

Imefahamika mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, anaweza kutambulishwa katika uwanja wa Villa Park baadae siku ya Jumanne kutegemeana na makubaliano ya uhamisho yatakavyokuwa yamekwenda.

Bent alijiunga na Sunderland akitokea Tottenham mwaka 2009, kwa ada ya awali ya paundi milioni 10, ambapo alisaini mkataba wa miaka minne.

Uhamisho wake huu unaonekana kuvunja rekodi ya awali iliyofanya Aston Villa, ilipomnyakua James Milner kwa paundi milioni 12, ambaye baadae akajiunga na Manchester City, lakini wakati huo akitokea Newcastle, na Stewart Downing alipochukuliwa kutoka Middlesbrough.

Kusajiliwa kwa Bent kutaonekana pia ni imani aliyonayo mmiliki wa Villa, Randy Lerner kwa meneja wao Gerard Houllier, licha ya Mfaransa huyo kuwa katika matatizo makubwa ya kuinyanyua klabu hiyo kutoka eneo la kushuka daraja, tangu achukue hatamu za kuingoza mwezi wa Septemba.

Kuondoka kwa mshambuliaji huyo ambaye timu yake ya Sunderland ipo nafasi ya sita ya msimamo wa ligi na kwenda katika timu inayoshikilia nafasi ya nne kutoka mkiani, kutamuacha meneja wa Sunderlad, Steve Bruce, kukabiliwa na kibarua kikubwa cha kuziba nafasi yake.

Bent, ambaye alianza kusakata kandanda akiwa na klabu ya Ipswich kabla ya kuhamia Charlton na Spurs, msimu uliopita alipachika mabao 25 na msimu huu hadi sasa ameshapachika mabao 11.

Bruce sasa atawategemea washambulaji wawili Asamoah Gyan na Danny Welbeck anayechezea kwa mkopo kutoka Manchester United.