Muuaji wa wanawake afungwa A kusini

Thozamile Taki
Image caption Thozamile Taki

Muuaji kutoka Afrika kusini amehukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la kuua wanawake 13.

Thozamile Taki, mwenye umri wa miaka 40, anayejulikana kama 'sugarcane killer' kutokana na kutupa miili ya wanawake hao kwenye mashamba ya miwa, na kuwalagahi kwa kuwaahidi kuwatafutia kazi.

Akimhukumu Taki kifungo cha maisha kwa kila kesi, Jaji King Ndlovu amemwelezea kama "mbweha kwenye ngozi ya kondoo."

Raia wa Afrika kusini wamefurahishwa na hukumu hiyo na kusifu jitihada za polisi.

Ndugu wa marehemu- baadhi ambao walikuwa wakimjua Taki binafsi-walilia na kushangilia wakati Jaji Ndlovu alipokuwa akisoma hukumu hiyo katika mahakama kuu ya Durban siku ya Jumatano mchana.

Jaji Ndlovu alisema, jinsi Taki alivyokuwa wakati wa kesi hiyo imechangia katika kutoa uamuzi wa kifungo hicho.

Alisema, " Hata waathiriwa walipolia hadharani wakati wa kutoa ushahidi, ulitabasamu tu."

Zaidi ya watu 100 walitoa ushahidi dhidi ya Taki wakati kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa mwaka 2009.

Miili ya wanawake hao iliyokuwa imeoza ilipatikana kwenye mashamba makubwa ya miwa na chai huko Umzinto, KwaZulu-Natal na Port St Johns mwaka 2007.

Taki amenyimwa haki ya kukata rufaa dhidi ya hukumu yake hiyo na anatarajiwa kupelekwa kwenye gereza lenye ulinzi wa hali ya juu huko KwaZulu-Natal.