Man United yaua, Arsenal yakandamiza

Manchester United ikionesha kiu ya ushindi, wameilaza Birmingham mabao 5-0, huku Dimitar Berbatov akifunga mabao matatu na mkongwe Ryan Giggs akifunga moja, akiwa msaada mkubwa kwa ushindi huo.

Image caption Berbatov akipachika moja ya mabao yake matatu

Berbatov alifunga bao la kwanza mapema katika sekunde ya 95 kwa mkwaju mkali baada ya Roger Johnson wa Birmingham kupoteza mpira. Bao la pili la Manchester United lilifungwa tena na Berbatov katika dakika ya 31

Mkongwe Giggs aliinua matumaini ya Manchester United kuutwa ubingwa na pia kutopoteza mchzo msimu huu, kwa kufunga bao zuri la tatu kabla ya mapumziko.

Berbatov aliyeonekana mwenye njaa ya kufunga mabao, alipachika bao la nne na la tatu kwake katika mchezo huo, baada ya kupokea pasi nzuri ya Giggs mara nyingine katika dakika ya 53, kabla Nani kuhitimisha karamu ya magoli kwa kupachika bao la tano dakika ya 76 na kuwaacha Birmingham wameishiwa mbinu zaidi.

Vinara hao wa Ligi, Man United wapo pointi mbili mbele ya Arsenal inayoshika nafasi ya pili, na rekodi yao ya kutopoteza mchezo kwamwe haiko hatarini baada ya Birmingham kuonekana haina nguvu ya ushindani.

Naye Robin van Parsie alifanikiwa kufunga mabao matatu peke yake na kuipatia timu yake ya Arsenal ushindi wa mabao 3-0 na pointi tatu dhidi ya Wigan katika uwanja wa Emirates.

Image caption Robin van Parsie akipachika moja ya mabao yake

Mlinda mlango wa Wigan Ali Al Habsi, aliwapa matumaini ya mapema wenzake kutokana na kuokoa mikwaju mikali ya wachezaji wa Arsenal, nafasi nzuri zaidi pale alipowanyima nafasi Cesc Fabregas na Van Persie.

Lakini Ali Al Habsi hata hivyo alishindwa kumzuia Van Persie kupachika bao la kwanza katika dakika ya 21, akiwa ndani ya sanduku la hatari na baadae katika dakika ya 58 alipopata pasi nzuri ya juu na ya mbali kutoka kwa Fabregas.

Van Persie alikosa kufunga mkwaju wa penalti, ambapo Gary Caldwell alitolewa nje kutokana na rafu aliyocheza na pia van Parsie mkwaju wake mwengine ukagonga mwamba wa lango, kabla hajaweka wavuni bao lake la tatu kwa mkwaju karibu na lango dakika ya 85.

Ushindi huo wa Arsenal umewawezesha kuwasogelea vinara wa ligi hiyo Manchester United na kusogea hadi nafasi ya pili kabla ya Manchester City waliokuwa wakishikilia nafasi ya pili hawajaingia uwanjani kuikabili Aston Villa. Arsenal hadi sasa wameweka kibindoni pointi 46.

Naye Kieran Richardson akisakata kandanda safi kipindi cha kwanza na kufunga mabao mawili peke yake, aliweza kuimarisha nguvu ya Sunderland kuwania nafasi ya msimu ujao kucheza kombe la Europa, baada ya kuwalaza Blackpool mabao 2-1.

Image caption Sunderland wakishangilia

Richardson alifunga bao la kwanza dakika ya 15 baada ya Sunderland kushambulia kwa kustukiza na alimalizia vizuri pasi ya Asamoah Gyan.

Alifunga bao lake la pili katika dakika ya 36 baada ya kazi nzuri ya Steed Malbranque.

Blackpool walipata bao la kufutia machozi kwa mkwaju wa penalti wa Charlie Adam katika dakika ya 86 na kufanya matokeo hadi mwisho mabao 2-1 kwa Sunderland.

Sunderland wamefika nafasi ya sita ya msimamo wa Ligi wakikusanya pointi 37.

Kwa upande mwengine Clint Dempsey alifunga mabao mawili yaliyoisaidia timu yake ya Fulham kukamilisha mchezo wa pili wa Ligi dhidi ya Stoke katika kipindi cha mwezi mmoja kwa ushindi.

Image caption Clint Dempsey akishangilia bado

Stoke walikuwa na nafasi nzuri ya kuongoza baada ya Ryan Shawcross mpira wa kichwa alioupiga kwenda nje na pia mkwaju wa Kenwyne Jones kugonga mwamba.

Matokeo hayo wamefika nafasi ya 14 wakiwa na pointi 26.

Bao la Marouane Fellaini katika dakika za nyongeza limeweza kuiokoa Everton na kuwanyima West Ham waliocheza wakiwa 10 nafasi ya kukwamuka kutoka mkiani baada ya timu hizo kutoka sare ya 2-2.

Image caption Marouane Fellaini akishangilia na wenzake wa Everton

Jonathan Spector aliipatia bao la kwanza West Ham baada ya pasi ya Luis Boa Morte, kabla ya Diniyar Bilyaletdinov kuisawazishia Everton.

Frederic Piquionne alijibu mashambulizi na kuipatia West Ham bao zuri la pili la kichwa kabla hajatolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kushangilia bila nidhamu bao hilo.

Matokeo hayo yanazidi kuibakisha West Ham mkiani wakiwa na pointi 21 na Everton wakiwa nafasi ya 13 na pointi 27.

Newcastle walishindwa kuhimili vishindo dakika za mwisho vya Tottenham, baada ya walinzi wake kumruhusu Aaron Leonnon awapite na kusawazisha, hali iliyofanya timu hizo kutoka sare ya 1-1 katika uwanja wa St James' Park.

Image caption Wachezaji wa Newcastle wakishangilia bao

Bao la Newcastle lilifungwa na mlinzi Fabricio Coloccini dakika ya 59 kipindi cha pili hali lililoweka matumaini makubwa kwa mashabiki wa timu hiyo wangeweza kunyakua pointi tatu.

Na Shola Ameobi, Peter Lovenkrands na Leon Best walikaribia kuipatia mabao Newcastle, kabla ya bao hilo la kuswazisha dakika za mwisho la Lennon.

Kwa sare hiyo Newcastle wamebakia nafasi ya saba wakiwa na pointi 30, huku Tottenham waking'ang'ania nafasi ya tano na pointi 30.