Asha na Eto Mlenzi wapata timu Uturuki

Mshambuliaji wa timu ya soka ya wanawake ya Mburahati Queens FC ya Tanzania, Asha Rashid anayechezea pia timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania- Twiga Stars, amewasili Istanbul, Uturuki, tayari kujiunga na klabu ya soka ya wanawake ya Atasehir Belediyespor, inayocheza ligi kuu ya soka ya wanawake Uturuki.

Image caption Asha Rashid na Rais wa klabu ya Atasehir, Sadik Kayhan

Iwapo Asha atafanikiwa katika upimaji wa afya yake na kupatiwa kibali cha kufanya kazi na serikali ya Uturuki, ataingia mkataba wa mwaka mmoja na nusu na klabu hiyo.

Klabu hiyo ya Atasehir Beladiyespor wanaongoza ligi ya wanawake ya nchi hiyo na iwapo watamudu kushikilia nafasi hiyo hadi mwisho wa msimu huu utakaomalizika mwezi wa Mei, watapata nafasi ya kushiriki mashindano ya kutafuta bingwa wa UEFA kwa vilabu vya Ulaya kwa wanawake msimu wa 2011/12.