Marekani yaiunga mkono Ivory Coast

Image caption Wafanyakazi wa Ivory Coast wakiweka mbegu za kakao kwenye magunia

Marekani imesema inaunga mkono wito uliotolewa na kiongozi wa Ivory Coast anayetambuliwa na jumuiya ya kimataifa Rais Alassane Ouattara wa kuzuia uuzaji wa kakao nje ya nchi kwa muda wa mwezi mmoja.

Kampuni ya kakao ya Marekani Cargill imesema "inasimamisha kwa muda" kununua mbegu ya zao hilo katika nchi inayozalisha kakao kwa wingi duniani.

Wito huo unatarajia kuongeza shinikizo ya kifedha kwa Laurent Gbagbo ili akiri kushindwa katika uchaguzi wa Novemba na kuachia madaraka.

Bei ya kakao- ambayo iliongezeka kwa asilimia 14 tangu uchaguzi- imeongezeka kwa asilimia nne siku ya Jumatatu.

Katika tukio jengine, Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema umoja wa mataifa usingemtambua Bw Ouattara haraka.

Msemaji wa Rais Tamale Mirundi aliliambia gazeti la Uganda la Daily Monitor, " Kunatakiwa kufanywe uchunguzi, siyo tu kutangazwa nani kashinda."

Awali Umoja wa Afrika uliiunga mkono umoja wa mataifa na chombo cha Afrika magharibi Ecowas imetishia kutumia nguvu kumtoa Bw Gbagbo iwapo atakataa kung'oka.