Kiongozi wa FDLR Rwanda apelekwa ICC

Waendesha mashtaka wa Ufaransa wamesema mkuu wa kundi la waasi la Rwanda anayeshutumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anasafirishwa kutoka Ufaransa kupelekwa Hague.

Callixte Mbarushimana alikamatwa mjini Paris mwezi Oktoba mwaka jana, kufuatia ombi lililotolewa na mahakama ya kimataifa ya ICC.

Image caption Callixte Mbarushimana

Kiongozi huyo wa waasi wa Kihutu amekana madai kuwa aliamuru wapiganajai wake wa FDLR kuua na kubaka raia.

Awali mahakama ya Kifaransa ilikataa rufaa dhidi ya yeye kuhamishwa lakini ilitoa uamuzi wa kutopelekwa Rwanda, ambapo mawakili wake walisema hatotendewa haki.

Bw Mbarushimana anakabiliwa na makosa matano ya uhalifu dhidi ya binadamu na makosa sita ya uhalifu wa kivita, ikiwemo makosa ya mauaji, unyanyasaji, ubakaji, matendo yanayoenda kinyume na binadamu, mateso, na uharibifu wa mali.