Rooney anahisii Chelsea ndio itawasumbua

Mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney amesema Chelsea wana uwezo wa kuihangaisha timu yake kuelekea kuutwaa ubingwa msimu huu.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wayney Rooney

Chelsea kwa sasa wako pointi 10 nyuma ya vinara wa ligi wa kuu ya England, Manchester United, lakini wameonekana kuimarika zaidi baada ya kushinda mechi zao tatu zilizopita na wametumia paundi milioni 70 kumnunua Fernando Torres na David Luiz.

"Bado hatujawaondoa Chelsea katika mbio za kuwania ubingwa," alisema Rooney, ambaye alipachika mabao mawili wakati Manchester United ilipowalaza Aston Villa 3-1 siku ya Jumanne.

"Chelsea ni timu kubwa, wapo imara na tunafahamu kama kuna yeyote atakayeweza kufanya vyema kuuchukua ubingwa basi ni wao."

Ameongeza: "Lakini tunafahamu, ni jukumu letu kuona taji linakwenda wapi na nina matumaini tunaweza kushinda."

Mabingwa hao watetezi Chelsea tayari msimu huu wamepoteza mechi mara sita na walionekana wamepoteza muelekeo wa kutetea taji lao, baada ya mfululizo wa kucheza ovyo na kushinda mechi moja tu kati ya tisa.

Lakini Chelsea, wanaonekana sasa kubadilisha kibao baada ya ushindi dhidi ya Blackburn, Bolton na Sunderland, na wanaweza pia kufanya vizuri zaidi siku zijazo kutokana na kuwa na mchezo dhidi ya Manchester United nyumbani na ugenini.

Wakati huo huo, Rooney ameonesha matumaini makubwa kwa kufunga mabao mawili dhidi ya Aston Villa, inaweza kuwa ndio mwanzo wa kurejea katika kiwango chake cha kupachika mabao.

Kabla ya mechi hiyo, Rooney anayechezea pia timu ya taifa ya England , alikuwa amefunga mabao mawili tu katika mechi za Ligi Kuu ya England.