Wenger amtetea Cecs kwa kauli ya Moyes

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger, amemtetea Cesc Fabregas baada ya meneja wa Everton David Moyes kutoa madai kwamba nahodha huyo wa Gunners alipaswa kutolewa nje wakati wa mapumziko.

Image caption Arsene Wenger

Everton walikuwa wakiongoza kwa bao 1-0 hadi kipindi cha kwanza, baada ya bao la utata lililofungwa na Louis Saha, aliyeonekana ameotea.

Lakini baada ya kupoteza mchezo kwa kufungwa mabao 2-1 katika uwanja wa Emirates, Moyes alisema: "Matamshi aliyoyatoa Fabregas kwa mwamuzi wa akiba na mwamuzi mwenyewe wakati wa mapumziko, alipaswa kutolewa nje kwa kadi nyekundu."

Hata hivyo Wenger alimtetea na kusema: "Fabregas hakuzungumza na mwamuzi wakati wa mapumziko, bali mimi ndiye nilizungumza naye."

Hasira zilipanda baada ya Saha kufunga bao la kwanza katika dakika ya 24 akiwa eneo ambapo mameneja wote walikiri alikuwa ameotea.

Hata hivyo, kwa mwamuzi Lee Mason kulikuwa na hamaki zaidi kwenye njia ya kuelekea vyumba vya kubadilishia nguo.

Moyes hakutaka kuzungumzia kile alichodai alisikia Fabregas akimwambia mwamuzi, lakini meneja huyo anahisi tukio hilo lilibeba matokeo ya mchezo.

"Nadhani kwa kutomtoa nje Fabregas kulibadili mtiririko wa mchezo," aliongeza Moyes.

"Nisingependa kutamka aliyoyasema Fabregas.

"Hayakuwa maneno mazuri kwa mtu mwenye hadhi na kipaji cha kusakata soka kama yeye.

"Kama angeyatamka maneno hayo uwanjani, angetolewa nje kwa kadi nyekundu."

Hata hivyo Wenger akimtetea nahodha wake alisema: "Nilikuwa karibu na Fabregas wakati wa mapumziko na sioni kwa nini David Moyes anamkasirikia."

Wenger alifurahishwa na moyo uliooneshwa na timu yake kuweza kurejesha bao na kupata la ushindi na kusema hali hiyo inaweza kuwasaidia katika mbio zao za kuutafuta ubingwa.

"Tupo tayari kwa mapambano ya kuwania ubingwa na tumeonesha hivyo kwa mara nyingine," Aliongeza Wenger.