Mancini ataka wachezaji wake kubadilika

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini amewataka wachezaji wake kubadilika kifikra baada ya kuongoza mara mbili na hatimaye kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Birmingham.

Image caption Roberto Mancini

City haijashinda michezo mitatu iliyopita na wapo pointi nane nyuma ya vinara wa ligi hiyo ya England, Manchester United, huku matumaini yao ya kutwaa ubingwa yakiyeyuka.

"Hatuna budi kubadilika. Tunahitajika kucheza soka yetu tena na tusahau yaliyotokea wiki mbili zilizopita," alisema Mancini.

Wachezaji wa Mancini walianza kwa mbwembwe wakati Carlos Tevez alipofunga bao la mapema, na licha ya Nikola Zigic kusawazisha, baadae kidogo Aleksandar Kolarov akafumua mkwaju wa free-kick na kuifanya City kuongoza kwa mabao 2-1 hadi mapumziko. Lakini Man City iliwabidi walipe gharama ya uzembe kwa mbinu zao za kupoteza muda, baada ya Craig Gardner kufunga bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti dakika za mwisho na kuisaidia Birmingham kuokota pointi moja.

Zimekuwa ni wiki mbili za ovyo ovyo kwa City, ambao iliwabidi wapate bao la dakika za mwisho lililofungwa na Edin Dzeko na kutoka sare dhidi ya Notts County katika mchezo wa kuwania kombe la FA wiki iliyopita, na kabla ya hapo walichabangwa 1-0 na Aston Villa katika mchezo wa Ligi Kuu ya England.

City kwa matokeo hayo wamejikuta nyuma kwa pointi tatu dhidi ya Arsenal wanaoshikilia nafasi ya pili na mchezo mmoja mkononi, wakati Chelsea walio nafasi ya nne wanaipumulia City kwa pointi mbili tu nyuma.