Benitez:Torres thamani yake £milioni 70

Aliyekuwa meneja wa Liverpool Rafael Benitez, amebainisha mpango wa paundi milioni 70 kwa uhamisho wa Fernando Torres ulianza mwaka jana, na pia angependa kuwa meneja wa klabu hiyo kwa mara nyingine.

Image caption Benitez na Torres

Torres alijiunga na Chelsea siku ya Jumatatu na kuvunja rekodi ya uhamisho nchini Uingereza ya kiasi cha paundi milioni 50, lakini thamani yake ingeweza kuwa ya juu zaidi.

"Nadhani mwaka jana tulikuwa tunazungumzia kiasi cha paundi milioni 70," Benitez alieleza alipohojiwa na BBC.

Benitez mwenye umri wa miaka 50, pia amesema angefurahi kuwa meneja wa Liverpool kwa mara nyingine siku zijazo.

Torres alijiunga na Chelsea katika siku ya mwisho ya dirisha dogo la usajili, ingawa Chelsea walianza kumuwania tangu mwezi wa Mei mwaka 2010. Licha ya kuumia goti mwishoni mwa msimu uliopita, alikuwemo katika kikosi cha Hispania kilichoshiriki kombe la dunia nchini Afrika Kusini.

Benitez alitimuliwa na klabu ya Italia ya Inter Milan mwezi Disemba, ikiwa ni miezi sita tu baada ya kutangaza anaondoka Liverpool kwa makubaliano ya pande mbili, baada ya kuwa meneja wa Liverpool kwa muda wa miaka sita.

Alifanikiwa kuiongoza Liverpool kubeba kombe la Ubingwa wa Ulaya mwaka 2005 na FA mwaka uliofuata, na alikuwa meneja wakati Torres alipojiunga na Liverpool akitokea Atletico Madrid kwa kitita cha paundi milioni 20 mwaka 2007.