Mashauriano ya kukabidhi madaraka Misri

Marekani imesema inafanya mashauriano na serikali ya Misri kuhusu utaratibu wa rais Hosni Mubarak kukabidhi madaraka.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maandamano eneo la Tahrir

Taarifa zinasema kuwa mojawapo wa masuala yanayozingatiwa ni Bw Mubarak kujiuzulu na kukabidhi mamlaka kwa baraza la kikatiba.

Serikali ya Marekani hata hivyo imesisitiza kuwa uamuzi kamili utatoka kwa watu wa Misri.

Wakati huo huo umati mkubwa wa watu umekusanyika kwenye eneo la wazi la Tahrir mjini Cairo wakishinikiza kuondoka mamlakani kwa rais Mubarak.

Ikilinganishwa na siku za awali, maandamano ya leo ni matulivu na waziri wa ulinzi Mohammad Hussein Tantawi ametembelea eneo hilo na kuwahutubia waandamanaji.

Kuna ulinzi mkali kwenye maandamano hayo huku wanajeshi wakishika doria.

Bw Mubarak alisema siku ya Alhamisi kuwa alihofia kutakuwa na machafuko iwapo ataondoka madarakani sasa.