Uwanja wa Soccer City gizani totoro

Uwanja mkubwa wa soka wa Soccer City nchini Afrika Kusini, ulioandaa fainali ya Kombe la dunia la kandanda mwaka 2010, hautaweza kuandaa mchezo wa ligi siku ya Jumamosi, kwa sababu wezi wameiba nyaya za umeme.

Image caption Uwanja wa Soccer City

Pambano la ligi baina ya Kaizer Chiefs wanaoshikilia nafasi ya pili na Moroka Swallows, limeahirishwa baada ya wezi kuiba nyaya zinazopeleka umeme uwanjani.

"Wizi wa nyaya katika maeneo jirani na uwanja huo, umesababisha kukosekana umeme na taa za uwanjani haziwaki na pia maeneo mengine ya uwanja huo hayana umeme," amesema msemaji wa ligi hiyo Altaaf Kazi.

"Hakuna umeme ofisini, vyumba vya kubadilishia nguo kwa wachezaji...hakuna umeme," aliongeza Kazi.

Mechi hiyo katika uwanja huo mkubwa wa michezo barani Afrika, sasa imepangwa kuchezwa tarehe 16 mwezi wa Februari.

Chiefs, ambayo ni klabu maarufu ya soka nchini Afrika Kusini, hivi karibuni ilihamishia mechi zake za nyumabni katika uwanja huo uliochezewa fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2010 kati ya Hispania na Uholanzi.

Wizi wa nyaya za shaba umeenea nchini Afrika Kusini, hali inayoathiri upatikanaji wa umeme, mawasiliano ya simu na huduma za reli na inakadiriwa kusababisha hasara ya mabilioni ya dola.

Uwanja huo wa Soccer City ulio nje kidogo ya jiji la Johannesburg, ulichezewa mechi kadha za Kombe la Dunia mwaka jana, ikiwemo pambano la ufunguzi kati ya Bafana Bafana na Mexico, robo fainali kati ya Ghana na Uruguay na pia fainali.