Misri yazidi kukumbwa na migogoro

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waandamanaji wanaopinga serikali ya Misri

Rais wa Misri Hosni Mubarak na familia yake wameripotiwa kuhodhi mali nyingi wakati wakiwa madarakani kwa kipindi cha miongo mitatu.

Kituo cha televisheni cha ABC nchini Marekani katika ripoti yake moja kilidai kuwa utajiri wa familia ya Mubarak unakisiwa kuwa ni dolla billioni 70.

Takwimu hizo zimenukuliwa na vyombo vya habari mbalimbali duniani. Lakini baadhi ya watu wanahisi kuwa taarifa hizo zimeongezwa chumvi.

Ikiwa familia ya Mubarak kweli wana utajiri huo wa dolla billioni 70, basi utakuwa sawasawa na na jumla ya tajiri mkubwa wa Mexico Carlos Slim na billionea wa kampuni ya Microsoft Bill Gates.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana za jarida la Forbes, watu hawa wawili ni nambari moja na mbili katika orodha za matajiri wakubwa duniani kila mmoja akiwa na dola billioni 35.

Haielekei kuwa familia ya Mubarak inafikia kiwango hicho. Lakini licha ya hayo bado wanaweza kuwa matajiri wakubwa.

Inaaminiwa wanamiliki nyumba za kifakhari katika maeneo kama Manhattan, Beverley Hills, California na eneo mashuhuri la matajiri la Belgravia jijini London.

Inaarifiwa kwamba familia ya Mubarak ina akiba ya fedha nyingi katika benki za Uingereza na Uswiz

Halikadhalika inasemekana wameelekeza fedha nyingi katika hoteli na sekta ya utalii katika bahari ya Sham.

Ni wazi kabisa Rais Hosni Mubarak amekuwa na fursa nyingi za kujitajirisha katika miaka 30 iliyopita kama mtu mwenye madaraka makubwa.

Wanawe Gamal na Alaa ni wafanyabiashara wakubwa nchini Misri na kabla ya kuzuka maandamano ya hivi majuzi Gamal alitajwa kama Rais mtarajiwa wa siku zijazo.

Kama kawaida taarifa si za uhakika na hazijathibitishwa; lakini si wengi watakaoshangazwa ikiwa familia ya Mubarak itajumuishwa katika fungu moja na familia za Marcos nchini Phillipines na Suharto wa Indonesia kama ni nembo ya ubepari uliokithiri--yaani familia za watawala katika nchi kubwa zinazoendelea ambazo zimefanikiwa kugeuza kuwepo kwao karibu na madaraka kuwa utajiri mkubwa binafsi.