Majangili watatu Afrika Kusini wameuawa

Majangili watatu nchini Afrika Kusini wameuawa na askari wa wanyama pori, katika hatua za hivi karibuni za kupambana na wawindaji haramu wa vifaru.

Image caption Vifaru wakiwa malishoni katika hifadhi ya taifa ya Kruger

Genge hilo lilikamatwa na kikosi cha usalama katika hifadhi ya wanyama ya Kruger, katika kipindi ambacho Afrika Kusini imeshuhudia matukio mia tatu ya uwindaji haramu mwaka jana.

Watuhumiwa watatu wa ujangili waliokuwa wakiwinda vifaru wameuawa na mmoja kujeruhiwa, baada ya kukabiliwa na askari wa wanyama pori katika hifadhi ya wanyama ya Kruger.

Kruger ni moja ya vivutio vikubwa nchini Afrika Kusini.

Askari wa wanyama pori wamesema wamekamata bunduki moja, risasi na vifaa vingine vinavyotumiwa kuwinda faru, katika eneo la tukio.

Soko la pembe za faru limeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, likichochewa na imani katika maeneo kadhaa ya Asia kuwa pembe hizo zina chembe chembe zenye tiba.

Katika soko lisilo rasmi bei ya pembe ya faru katika eneo hilo inauzwa kwa takriban dola elfu hamsini na tano kwa kilo moja.

Mwaka jana pekee, Afrika Kusini ilishuhudia matukio mia tatu ya ujangili, na licha ya kuwepo kwa ahdabu kali za kisheria, bei kubwa ya pembe hizo inasaidia kuchochea biashara hiyo.