Upinzani Yemen wamshinikiza rais Saleh

Haki miliki ya picha ap
Image caption Wananchi wakiandamana nchini Yemen.

Upinzani nchini Yemen unasema unasubiri Rais Ali Abdullah Saleh, kutimiza ahadi alizotoa wiki iliyopita wakati wa maandamano yaliyochochewa na matukio nchini Tunisia na Misri.

Bwana Saleh alisema hatagombea tena kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2013 na kuwa hatamuachia mwanawe mamlaka.

Pia ameahidi mageuzi kabambe ya kiuchumi na kisiasa.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha kisocialisti nchini Yemen Yassine Nomani amesema kuwa maandamano nchini Misri yamebadilisha joto la kisiasa nchini Yemen.

Katika mahojiano na BBC amesema hii ni mara ya kwanza kwa muda wa miongo mingi kwa upinzani kuwa na nafasi ya kumshinikiza rais kutekeleza mabadiliko.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais Abdullah Saleh wa Yemen.

Rais Ali Abdullah Saleh ambaye amekuwa mamlakani kwa zaidi ya miaka 30 anakabiliwa na upinzani mkubwa.

Ufisadi unadaiwa kukithiri nchini humo na pia kumekuwa na matatizo uhuru wa kujieleza.

Rais huyo ni mshirika wa karibu wa Marekani ambayo imeipa nchi hiyo mamilioni ya dola ili kusaidia katika vita dhidi ya Al Qaeda.

Hatua ya Rais huyo kutangaza kuwa hatagombea urais mwa 2013 inaonekana kutuliza vyama vya upinzani ambayo vinasema vinasubiri kuona kama atatimiza aliyoahidi hivi karibuni.