Arnesen atetea kununuliwa kwa Torres

Mkurugenzi wa michezo wa Chelsea Frank Arnesen, ametetea klabu hiyo kumnyakua Fernando Torres, akisema hiyo haiwazuii kukuza vipaji vyao wenyewe.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Fernando Torres

Torres, mwenye umri wa miaka 26, alijisajili Chelsea akitokea Liverpool kwa kitita cha paundi milioni 50, tarehe 31 mwezi wa Januari, ikiwa ni siku hiyo hiyo mchezaji mwengine wa Chelsea, Daniel Sturridge alipojiunga na Bolton kwa mkopo.

Lakini Arnesen, ambaye ndiye mwenye jukumu la chuo cha kukuza vipaji katika klabu hiyo, ameiambia BBC: "Kumsajili Torres ni jambo zuri sana."

"Kwa sababu kusajili mchezaji haina maana mlango umefungwa kwa wengine."

Arnesen amekuwepo katika klabu ya Chelsea tangu mwaka 2005 akitokea Tottenham in 2005 na atastaafu nafasi yake mwishoni mwa msimu huu.

Ameongeza:"Tunapaswa kuhakikisha vijana wengine wapo vizuri wakati utakapowadia na hilo litatokea tu, hakuna mashaka yoyote."

Chelsea imekuwa ikishutumiwa kwa kutumia pesa nyingi kwa wachezaji, zaidi ya kukuza vipaji vipya kupitia chuo chao, ambacho ni bora katika Ligi Kuu ya England.

Klabu hiyo msimu uliopita ilishinda kombe la FA kwa vijana, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1961, na kiungo Josh McEachran mwenye umri wa miaka 17, amekuwa akitumiwa mara kwa mara na meneja Carlo Ancelotti katika timu ya kwanza.

Nahodha John Terry ndiye mchezaji wa mwisho katika klabu hiyo kuweza kujipenyeza hadi kikosi cha kwanza na Sturridge, mwenye umri wa 21, ameshindwa kuwemo katika kikosi cha kwanza mara kwa mara tangu alipojiunga na klabu hiyo akitokea Manchester City mwaka 2009.

Kufuatia kwenda Bolton, ambapo atakuwepo hadi mwishoni mwa msimu huu, Sturridge ameshafunga mabao mawili katika mechi mbili alizocheza.

Zaidi ya kumsajili Torres siku ya mwisho ya usajili wa dirisha dogo, Chelsea pia imeilipa klabu ya Benfica kiasi cha paundi milioni 21 kwa mlinzi Mbrazil, David Luiz.