Kampeni Uganda zanazidi kupamba moto

Kampeini za Urais nchini Uganda bado zinaendelea licha matatizo madogo ya hapa na pale kuwahusu wagombeaji wa kiti hicho.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Yoweri Museveni wa Uganda

Huku mgombea mmoja akiwa hospitalini baada ya kufanyiwa upasuaji wengine wanaendelea na mikutano ya kampeini japo wanasumbuliwa katika mikutano hiyo, mfano mmoja inasemekana amezomewa na vijana wa upinzani na vijana hao kukamatwa.

Muda wa siku za kampeini za uchaguzi wa Urais na ubunge ukiwa unayoyoma, na wahusika wamezidisha juhudi za kutafuta kura. Kampeini zinapashwa kumalizika tarehe 16 mwezi huu wa Februari. Siku ya Jumanne baadhi ya wagombea walipaswa kufanya kampeni katika sehemu tofauti. Mgombea wa kiti hicho akitumia tiketi ya chama tawala cha National Resistance Movemen-NRM-Yoweri Museveni, alikuwa amepangiwa kufanya mkutano wa kampeini katika eneo la Buganda wilaya ya Wakiso ambayo ni jirani na wialya ya jiji kuu ya Kampala.

Kuna taarifa mgombea huyo, katika mkutano mmoja alizomewa na baadhi ya watu waliokuwa wakimsikiliza. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uganda, vikimnukuu msemaji wa Polisi Bi Judith Nabakooba, watu sita wamepelekwa rumande katika magereza yaliyoko katika wilaya jirani ya Mpigi.

Watu hao inasemekana walimzomea Rais Museveni wakati akifanya mkutano wa kampeini katika soko moja eneo la Buwama. Vyombo vya habari vinamnukuu afisa polisi aliyeshudia mkasa hicho akisema kundi la vijana ambao walionekana kama wa vyama vya upinzani, walianza kumzomea punde tu alipoanza kuhutubia mkutano huo. Miongoni mwa maneno waliokuwa wakitumia ni kama tumekuchoka, umekuwa madarakani kwa muda murefu pamoja na mengine.

Taarifa zingine zinasema waliokamatwa kutokana na sakata hilo wanafikia 20. Hata hivyo msemaji wa polisi Bi Nabakoba ameiambia BBC kwa simu kuwa asitoe kauli yoyote kuhusu suala hilo.

Hii inaonekana kama mara ya kwanza jambo kama hilo likimtokea Museveni tangu kampeini zianze. Na hayo yakiarifiwa mgombea mwingine wa kiti hicho na mwanamke pekee, Betty Oliva Kamya wa chama kipya cha Uganda Federal Alliance, ambae kwa mujibu wa ratiba alikuwa ahuhutubie eneo la magharibi mwa Uganda, lakini hakufanya hivyo kutokana na ushauri wa madaktari ambao walimfanyia upasuaji wa tumbo.

Haijulikani ikiwa hilo litathiri kampeini zake. Wengine kama vile Nobert Mao wa DP; Kiiza Besigye wa IPC; Jaberi Bidandi Ssali wa PPP, Dr Abed Bwanika wa PDP, Olara Ottunu wa UPC na mgombea wa kujitegemea Walter Samuel Lubega wao wameendelea kutafuta kura katika sehemu tofauti nchini.