Maharamia wateka meli ya Italia

Jeshi la wanamaji la Italia limesema maharamia wamekwea na kuchukua udhibiti wa meli ya mafuta ya Italia katika bahari ya Hindi.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Meli ya Ujerumani ambayo pia imetekwa

Maharamia hao walifyatua risasi katika chombo kiitwacho Savina Caylyn, takriban kilomita 800 kutoka pwani ya Somalia.

Msemaji wa jeshi la wananamaji amesema hakuna aliyejeruhiwa miongoni mwa mabaharia 17 kutoka India na wataliano watano.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maharama wamejipatia mamilioni ya dola

Msemaji wa jeshi la wanamaji la Umoja wa Ulaya amesema shambulio la chombo hicho limefanyika katika eneo la mashariki mwa kisiwa cha Yemen cha Socotra.

Meli hiyo imebeba shehena ya mafuta yaliyokuwa yakipelekwa katika bandari ya Pasir Gudang nchini Malaysia, limeripoti shirika la habari la Reuters.

Image caption Wanajeshi wa Marekani wakiwa na maharamia

Meli ya kivita ya Italia ilikuwa ikielekea katika eneo la tukio, lakini iko umbali wa kilomita 600, na inatarajia kuchukua siku kadhaa kuwasili, limeripoti shirika la habari la Italia.

Umoja wa Ulaya umesema meli hiyo imetekwa na mashua moja ikiwa na maharamia watano.

Image caption Maharamia wa Somalia

Msemaji wa jeshi la wanamaji wa Umoja wa Ulaya amesema meli hiyo "ilikuwa ikielekea magharibi," upande wa pwani ya Somalia, shirika la habari la AFP limekaririwa.

Maharamia wa Kisomali wametjipatia mamilioni ya dola katika miaka ya hivi karibuni kwa kuteka meli za mizigo katika njia inayotumiwa na meli katika pembe ya Afrika.