Walcott aonya wenzake kwenye Twitter

Mshambuliaji wa Arsenal Theo Walcott amesema wachezaji "wanaanza kujichimbia kaburi lao wenyewe" kwa kutuma ujumbe wa lawama kwa waamuzi kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Image caption Theo Walcott

Baada ya Gunners kwenda sare na Newcastle siku ya Jumamosi, Jack Wilshere alitumia mtandao wa Twitter kueleza maoni yake juu ya waamuzi "kuonekana kutetereka".

Lakini Walcott amesema: "Hakuna sababu ya kupima uwezo wa waamuzi baada ya mchezo. Kufanya hivyo hakuwezi kubadilisha matokeo.

"Kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake, lakini unatakiwa kuwa makini kwa kile unachofanya kwa kuzingatia maisha yako binafsi."

Wilshere alituma maoni yake kupitia Twitter kuonesha hasira zake kwa mwamuzi Phil Dowd wakati wa mechi iliyochezwa uwanja wa St James' Park, ambapo Newcastle walipigana kiume baada ya kuwa nyuma kwa mabao 4-0 na kulazimisha sare ya mabao 4-4, ambapo pia walipata mikwaju miwili ya penalti.

Walcott alisema yeye mwenyewe hatumii twitter na hajui hata inavyofanya kazi na wala haipendi.

Wilshere baadae akayaondoa maoni hayo na baada ya kuchunguza suala lenyewe, Chama cha Soka cha England, kikaamua kutomuadhibu mchezaji huyo, ambaye pamoja na Walcott wamo katika kikosi cha timu ya taifa ya England kitakachopambana na Denmark mjini Copenhagen siku ya Jumatano.

Mchezaji wa zamani wa Liverpool Ryan Babel alitozwa faini ya paundi 10,000 na FA mwezi wa Januari, baada ya kutuma picha aliyoitengeza ya mwamuzi Howard Webb akiwa amevaa fulana ya Manchester United, baada ya Liverpool kufungwa bao 1-0 katika uwanja wa Old Trafford wakati wa patashika za kuwania Kombe la FA.