Pep Guardiola kuongeza mkataba Barcelona

Kocha wa Barcelona Pep Guardiola amekubali kuongeza muda wa kuifundisha timu hiyo hadi mwisho wa msimu ujao.

Image caption Pep Guardiola

Mkataba wa sasa wa Guardiola unamalizika mwishoni mwa msimu huu wa ligi, na Barcelona kwa sasa wamo mbioni kuongeza mkataba wake kutokana na mafanikio aliyoyapeleka katika klabu hiyo.

"Mkataba huo mpya utatiwa saini siku zijazo," taarifa hiyo ya klabu imesema.

Guardiola ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 40, ameshinda mataji manane, ikiwemo kutetea taji la Ligi ya nchi hiyo maarufu La Liga na ubingwa wa vilabu vya Ulaya mwaka 2009, tangu aliposhika hatamu za kufundisha klabu hiyo kutoka kwa Frank Rijkaard mwaka 2008.

Barca kwa sasa wanaongoza La Liga wakiwa mbele kwa pointi saba na siku ya Jumapili, ilikuwa ni klabu ya kwanza kushinda mechi 16 za La Liga mfululizo baada ya kuilaza Atletico Madrid 3-0.

Guardiola ataanza tena hekaheka zake za kuwania ubingwa wa vilabu Ulaya kwa mara ya pili akiwa kocha wa Barcelona, watakapokabiliana na Arsenal katika mchezo wao wa awali wa timu 16 utakaochezwa uwanja wa Emirates, tarehe 16 mwezi huu wa Februari.

Akiwa amevutia baada ya kuifundisha vizuri timu ya pili ya Barcelona, Guardiola alichaguliwa kuwa kocha wa timu ya kwanza wa Nou Camp mwishoni mwa msimu wa 2007-2008.

Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa Hispania, ametokea katika mfumo wa timu ya vijana wadogo ya Barca, ameshinda mataji sita ya ligi na moja la Ulaya akiwa anachezea Barcelona.