Ukame waathiri wanafunzi Kenya

Haki miliki ya picha peter njoroge
Image caption Mto umekauka Lodwar, Kenya

Shule nyingi katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa Kenya karibu na Ziwa Turkana, kwa kawaida hutoa chakula katika shule zao za msingi.

Chakula hiki huwavutia watoto wengi kuhudhuria elimu katika eneo hilo, ambalo lina jua kali na mvua kidogo sana kwa mwaka mzima.

Mfano mzuri ni shule ya msingi ya Lokichare, karibu na mji wa Lodwar, unaonyesha kuwa chakula siku hizi hakipatikani katika shule nyingi.

Wanafunzi wanaojitokeza kuwakaribisha waandishi wa BBC katika shule yao wanaimba wimbo katika lugha asilia ya eneo hilo, Kiturkana, ambao unaeleza umuhimu wa kuosha mikono.

Cha kushangaza ni kuwa hakuna chakula wala maji ya kunywa sembuse maji ya kunawa. Mito na visima vimekauka.

Mashirika yasiyo ya kiserikali yametoa chakula kwa serikali ili kisambazwe mashuleni.

Lakini mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Lokichare, Edward Lodoso Somal, amesema tangu shule kufunguliwa mapema mwezi wa Januari, hakuna chakula chochote kilichopelekwa katika shule hiyo.

"Nadhani chakula hakijafika shuleni kwa sababu ya ukosefu wa uchukuzi," Anasema huku akiwa amesimama katika jengo dogo linalotumiwa kama jiko, lililojaa kuni na moshi lakini bila chakula cha kupika.

Rose Ogola, afisa habari wa shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula (WFP), amethibitisha kuwa tayari chakula kimegawanywa katika shule mbalimbali kwenye maeneo kame kama Lodwar na Turkana.

"Tunashangazwa kuwa hakuna chakula katika shule hiyo unayoitaja na sisi tayari tumekitoa chakula kwa shughuli hizo," Afisa huyo alieleza.

Ukame na wanafunzi

Kusafiri hadi Lodwar huchukua muda wa siku mbili, mwendo wa kilomita 700 kutoka Nairobi, kwenye barabara mbovu. Mwendo huu mrefu unatatiza serikali katika shughuli zake za kutoa chakula kwa taasisi mbalimbali.

Bwana Somal anasema mwaka uliopita alikuwa na wanafunzi 280 lakini kwa wakati huu ana watoto 90 pekee.

Idadi kubwa ya wanafunzi wasio shuleni waliandamana na wazazi wao kwenda kwenye malisho ya mifugo yao nchini Uganda, Sudan na Ethiopia.

Wengine wamehama kutoka vijijini hadi vituo vya kibiashara wakitarajia kupata chakula kwa urahisi zaidi.

Ukame si jambo geni nchini Kenya. Ukame mbaya zaidi nchini Kenya wa hivi karibuni ulitokea miaka miwili iliyopita. Bwana Somal anapendekeza kuwa serikali inapaswa kuwa na mikakati ya muda mrefu kukabiliana na madhara ya ukame.

"Wachungaji wanapaswa kuhimizwa kuuza mifugo yao wakiwa wangali na afya na wanono na kuweka pesa zao katika benki ili wazitumie baadaye kununua mifugo wakati wa msimu wa mvua unaporudi," Anaeleza.

Katika kiangazi cha 2009 wakati serikali ilipotangaza kutaka kununua mifugo kutoka kwa wachungaji ili kuwapunguzia makali ya ukame, wengi wao walikataa wakitarajia kuwa mvua ingenyesha wakati ule.

Hata hivyo, haikunyesha na wakati walipokubali kuuza mifugo yao, walikuwa dhaifu sana hivyo wengi wao walikufa njiani walipokuwa wakisafirishwa hadi kichinjio cha kitaifa cha KMC kilichoko kitongoji cha mji wa Nairobi.

Ukame waathiri wanyama

Mtu anapoendesha gari katika eneo la Turkana, kile anachoona zaidi ni changarawe na vichaka vichache vya miti aina ya mgunga 'Acacia' ambayo mbuzi na ngamia wanatumia kama chakula.

Wavulana na wazee wanaonekana kandokando mwa barabara kuu wakiomba maji kwenye barabara hiyo ambayo joto lake hufika zaidi ya nyuzi joto 40.

Katika eneo la Kalotum, kilomita 15 kaskazini mwa mji wa Lodwar, tuliingia katika boma moja ambako tuliwakuta wanawake na watoto wakiishi.

Haki miliki ya picha peter njoroge
Image caption Waturkana wameamua kuchimba kisima cha maji wanchotumia na wanyama waliobaki

Karibu nao tuliona mbuzi watatu waliokonda waking'ang'ania takataka iliyokuwa karibu na mimea ya mgunga.

Leah Lokala, mwenye umri wa miaka 27, ndiye pekee aliyeweza kuongea Kiswahili, ishara kuwa amewahi kupata elimu, angalau kwa miaka kadhaa.

"Kiangazi kimewaua ng'ombe wetu wote na kwa wakati huu tuna mbuzi watatu pekee na hata hawa mbuzi watatu tunalazimika kutembea kwa zaidi ya kilomita 15 kuwatafutia maji ya kunywa," Leah alisema.

Mwendo wa kilomita kadhaa kutoka mji wa Lodwar tukiendelea Ziwa Victoria, tuliona ngamia mmoja amekwama kwenye changarawe. Ishara hii si nzuri kwa sababu yeyote anayejua historia ya ngamia anafahamu kuwa iwapo kuna mnyama anayeweza kustahimili ukame katika mazingira magumu zaidi ni ngamia.

Katika jamii za Pokot na Turkana, wengi wanafahamu kuwa maisha yatakuwa magumu wakati wowote ule wanaposhuhudia ngamia na mbuzi wakifa kwa sababu ya jua.

Wanyama hawa wawili wanatambuliwa kama wanyama wakakamavu zaidi katika eneo hilo.

Jamii hizi za wafugaji zinazoishi katika maeneo yanayopakana na Uganda, Sudan, Ethiopia na hata Somalia zinafahamu kuwa majirani wao wakipoteza mifugo yao kutokana na kiangazi; huwa wana tabia ya kuiba mifugo kutoka kwa jirani zao kwa sababu hawawezi kwenda sokoni kwa kukosa pesa.

Mashirika mengi yasiyo ya kiserikali na serikali ya Kenya yameanzisha kampeni kali ya kuomba chakula cha kuwakomboa wakazi wa maeneo hayo kame.

Wakati huo huo serikali inajitahidi kuelimisha jamii zinazopakana umuhimu wa kuheshimiana ili kunapotokea maafa haya waweze kutumia kwa pamoja.

Chama cha Msalaba Mwekundu cha Kenya kinasema kwa wakati huu zaidi ya Wakenya milioni mbili na mifugo zaidi ya milioni 20 wanahitaji chakula cha ziada kabla ya msimu wa mvua ambao kwa wakati huu wakazi wa maeneo hayo, hawajui utarudi lini.