Polisi amshitaki Winnie Mandela

Afisa mmoja wa polisi nchini Afrika Kusini amefungua mashitaka dhidi ya mke wa zamani wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Chama cha wafanyakazi cha polisi huyo kimesema hatua hiyo imefikiwa baada ya polisi kumtuhumu Winnie Madikizela-Mandela kwa kuendesha gari kwa kasi.

Haki miliki ya picha none
Image caption Winnie Mandela

Chama hicho, Solidarity kimemtuhumu Winnie kwa kujaribu kumtisha polisi huyo Jannie Odendaal.

Anatuhumiwa kwa kuvunja sheria, kujeruhi na kuendesha gari kwa uzembe.

Bw Ondendaal pamoja na askari mwenzake walikuwa tayari wamehamishiwa katika nafasi nyingine.

Dereva wa Winnie na mlinzi wake binafsi wamewasilisha malalamiko yao ya kutishwa na kuelekeza bunduki dhidi ya wawili hao.

Uchunguzi umeanza kuhusu mwenendo wao.

Kasi

Solidarity imesema Bw Odendaal alikuwa akitekeleza wajibu wake.

"Madikizela-Mandela na walinzi wake ndio walitakiwa wachunguzwe kwa mienendo yao," amesema Dirk Hermann, katibu mkuu wa chama cha Solidarity, katika taarifa aliyotoa.

Bi Madikizela hajasema lolote kuhusiana na sakata hilo.

Bw Odendaal, ambaye alisimamisha gari la Madikizela-Mandela mwezi Disemba, amesema alikuwa akiendesha gari kwa kasi ya kilomita 150 kwa saa, ambayo ni kilomita 30 zaidi ya kasi inayoruhusiwa.