NATO yakamata mashua ya maharamia

Kikosi cha NATO kinachoshughulikia tatizo la uharamia kimesema, meli yao ya kivita imeinasa mashua kuu ya maharamia karibu na mwambao wa Somalia.

Image caption Meli ya kivita ya Denmark

Meli hiyo ya kivita kutoka Denmark ilifyatua risasi siku ya Jumamosi kama onyo na kuilazimisha mashua hiyo kusimama na mabaharia wake kujisalimisha.

Watuhumiwa kumi na sita waliokuwa kwenye mashua hiyo walikamatwa na silaha zilizokuwa zimefichwa humo kunaswa pia.

Mateka wawili raia wa Yemen waliokuwa ndani ya mashua hiyo pia waliachiwa.

'Mashua hizo zinawapa maharamia mahali pa kuegesha majini. Zinaleta tishio kubwa kwa meli za bidhaa,' Kamanda Haumann wa meli hiyo ya kivita ya HDMS Esbern Snare alisema.

Kikosi hicho cha NATO kilisema tukio hilo lililfanyika siku ya Jumamosi asubuhi wakati meli ya Denamark ilipokutana na chombo kilichokuwa kimebeba mashua ndogo nyepesi na kuwatilia mashaka.

Walishuku kuwa chombo hicho kilikuwa kimetekwa nyara.

Mamilioni ya dola

Jeshi la majini la Jumuiya ya Ulaya pamoja na kikosi cha NATO, wamekuwa wakisindikiza meli za bidhaa katika Ghuba ya Eden tangu mwaka wa 2008.

Mapema wiki hii, Umoja wa wamiliki wa meli za mafuta walisema maharamia kutoka Somalia wameziteka meli takriban ishirini na kuzitumia kuwashambulia mabaharia.

Maharamia wa Somalia wamepata mamilioni ya dola katika miaka ya hivi karibuni kwa kuziteka nyara meli za bidhaa karibu na Pembe ya Afrika, na kudai kulipwa fedha za kikombozi.

Somalia haijakuwa na serikali dhabiti tangu mwaka wa 1991 na haina uwezo wa kudhibiti tatizo hili la maharamia.