Kampuni ya Chevron yatozwa faini ya $8B

Uchafu unaodaiwa kusababishwa na kampuni ya Chevron Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Uchafu unaodaiwa kusababishwa na kampuni ya Chevron

Mahakama moja nchini Ecuador, imetoza kampuni ya mafuta ya Chevron faini ya $8B kwa kuchafua mazingira katika eneo kubwa la Amazon nchini humo.

Wakili wa walalamishi, Pablo Farjado, alilaumu kampuni ya Texaco iliyoungana na Chevron mwaka 2001 kwa kuyachafua hali ya mazingira katika misitu Kaskazini mwa Ecuador kuanzia mwaka 1972.

Kampuni hiyo ya Chevron imesema inajadili uwezekano wa kukata rufaa.

Farjardo amesema kuwa mimea iliharibiwa na maji ya kunywa kuchafuliwa kitendo ambacho kilisababisha raia katika eneo hilo kukumba na mateso mengi.

Chevron, kwa upande wake, imesema kuwa uamuzi huo wa mahakama ni mgumu kutekeleza na kwamba watakata rufaa.

Msemaji wa chevron, Kent Robertson, aliambia BBC kuwa Texaco ilisafisha maeneo yote yaliyochafuliwa baada ya kumaliza shughuli zake nchini Ecuador na inalaumu kampuni ya serikali ya Petro-Ecuador kwa kuendelea kuchafua maeneo hayo baada ya Texaco kuondoka.