Ubingwa Ulaya Arsenal yairarua Barca 2-1

Arsenal ikishambulia kwa nguvu katika muda wa dakika tano kipindi cha pili, walifaulu kurejesha bao na kupata la ushindi dhidi ya Barcelona, wanaopewa nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa wa soka kwa vilabu vya Ulaya, pambano lililochezwa uwanja wa Arsenal wa Emirates.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Robin Van Parsie akishangilia bao la kusawazisha

Barcelona walionekana kupania kutafuta ushindi wa mapema na kulinda ushindi wao kwa bao la kipindi cha kwanza lililofungwa na mshambuliaji hatari David Villa, wakijiandaa kwa pambano la marudio litakalochezwa uwanja wa Nou Camp.

Barcelona walipoteza nafasi kadha ambazo wangezitumia wangeimarisha nafasi yao, huku Lionel Messi akiwa amekosa nafasi nyingi zaidi ya wenzake, akikosa kupachika bao wakati lango la the Gunners lilipokuwa wazi na kwa mastaajabu ya wengi akaupiga mpira nje.

Robin van Persie alisawazsiha kwa mkwaju mkali alipoupiga kiufundi akiwa katika sehemu ambayo si rahisi kufunga na kumuacha mlinda mlango wa Barcelona, Victor Valdes akishindwa kulinda lango vizuri na kuachia upenyo, kabla ya Andrey Arshavin aliyeingizwa kipindi cha pili kupachika bao la pili na kuwafanya mashabiki wa Arsenal wakipagawa kwa shangwe zisizo kifani, wakiwa na wanajiamni sasa watakapokwenda kwa pambano la marudiano nchini Hispania.

Arsenal walikuwa wanafuata nyayo za wapinzani wao katika Ligi Kuu ya England, Tottenham baada ya kuwalaza AC Milan kwenye uwanja wa San Siro siku ya Jumanne.

Kocha wa Barca Pep Guardiola bado anayo matumaini ya kugeuza matokeo hayo katika pambano la marudiano, lakini the Gunners sasa wanacho kitu cha kujilinda na watasafiri kwenda Hispania wakiwa wanajiamini.

Jack Wilshere alikuwa kioo cha maendeleo mazuri ya Arsenal tangu timu hizo mbili zilipokutana kutokana na kuwadhibiti kikamilifu wachezaji hatari wa kiungo wa Barcelona.

Meneja wa Arsenal, Wenger ameelezea pambano hilo ulikuwa "usiku maalum" - na meneja huyo wa Arsenal hana budi kupongezwa kutokana alivyogeuza matokeo ya mpambano huo kwa mabadiliko aliyofanya kwa kumuingiza Arshavin badala ya Alex Song na Nicklas Bendtner akichukua nafasi ya Theo Walcott licha ya kwamba timu yake ilikuwa nyuma kwa bao 1-0.