Wito wa 'siku ya ghadhabu' Libya

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watolewa na wanaharakati kupitia mitandao ya kijamii

Wanaharakati wanaopinga serikali nchini Libya wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kupata watu wa kuwaunga mkono kwenye maandamano ambapo wanaelezea kama "siku ya ghadhabu."

Kulikuwa na ripoti za mapigano katika miji miwili siku ya Jumatano, huku takriban watu wanne wakiripotiwa kufariki dunia katika mji wa al-Bayda mashariki mwa nchi hiyo.

Idadi kubwa ya watu walijeruhiwa katika maandamano yaliyo na vurugu siku ya Jumanne usiku katika mji wa Benghazi.

Ghasia hizo zimeibuka baada ya mkosoaji wa serikali kutiwa kizuizini.

Maandamano ya kuunga mkono demokrasia hivi karibuni yameenea katika mataifa ya kiarabu, huku marais wa Tunisia na Misri walipolazimika kujiuzulu kutokana na ghasia hizo.

Lakini maandamano ya wiki hii ni mara ya kwanza kuonyesha ujasiri wa kweli nchini Libya, nchi ambayo kupingwa hakustahamiliwi.