Tume ya uchaguzi Uganda yatoa maelekezo

Kampeni za uchaguzi mkuu wa Urais pamoja na wabunge nchini Uganda zilimalizika rasmi na sasa tume ya uchaguzi imetoa maelezo kuhusu uchaguzi wa kesho.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mfanyakazi wa Tume ya uchaguzi Uganda

Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi kipindi cha kutafuta kura kwa wagombea Urais na ubunge kilikuwa kati ya tarehe 28 mwezi wa Oktoba mwaka 2010 hadi tarehe 16 mwezi wa Febuari mwaka huu wa 2011. Hivyo mkuu wa tume ya uchaguzi nchini Uganda, Mhandisi Badru Kigunddu, akihutubia waandiahi habari wa ndani na nje,katika makao makuu ya tume hiyo ,ametoa ushauri kwa wagombea viti hivyo.

Asema kufuatia muda wa mwisho wa kampeni kumalizika,tume inawahimiza wagombea kusitisha mikutano yote ya hadhara pamoja na mikutano na waandishi habari yenye nia ya kutafuta kura kwa viti vya urais na ubunge.

Kuhusu matayarisho ya upigaji kura wa siku ya Ijumaa mkuu wa tume ya uchaguzi amesema tume yake imekamilisha usambazaji wa vifaa vitakavyo tumika katika wilaya zote 112.

Ameongeza kuwa vifaa hivyo vitasambazwa kutoka makao makuu ya wilaya hadi tarafa ndogo , ambapo wakuu wa vituo vya kupigia kura watavichukua mapema asubuhi. Pia amesema matayarisho yote yanayohitajika kuona kama vituo vyote vya kupigia kura nchini vipatavyo 23,968 vitakuwa na vifaa vya kutumiwa na kuanza kwa wakati. Ameongeza kuwa ni wale tu ambao waliandikishwa katika daftari la kupigia kura ndio pekee watakaokubaliwa.

Upigaji kura unaanza saa moja asubuhi na kumalizika saa kumi na moja jioni.