Besigye alalamika Uganda

Mgombea urais wa upinzani nchini Uganda ameelezea uchaguzi mkuu nchini humo kuwa ni "kashfa ya kushtua" akidai kuwepo njama ovu za kuiba kura.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Adai uchaguzi ulikuwa ni "kashfa ya kushtua"

Akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi jioni mjini Kampala, Kizza Besigye wa muungano wa vyama vya kisiasa, Inter-Political Parties (IPC), alimshtumu Rais Yoweri Museveni, jeshi na polisi kwa kuhusika na kile alichokieleza "Kashfa ya kushtua".

Kwa mujibu wa Besigye, "mazimwi walipiga kura katika uchaguzi huo kwa kuwa daftari la wapigaji kura limejaa majina hewa".

Besigye, ambae aliwahi kuwa daktari binafsi wa Rais Museveni, alidai kwamba vikosi vingi vya kijeshi vilipelekwa wakati wa mchakato wa uchaguzi na kusambazwa katika pembe zote za nchi hiyo "vikitishia kuzuka vita "ikiwa Rais Museveni hatashinda uchaguzi huo.

Besigye alisema ameitisha mkutano wa viongozi wa muungano huo wa vyama ili"waamue wachukue hatua gani".

Aliongeza kusema kwamba upinzani "hautakwenda mahakamani kwa kuwa nguvu ya mwisho iko mikononi mwa wananchi ".

Matokeo ya awali yanaonyesha Rais Museveni anaelekea kupata ushindi huku Besigye akishikilia nafasi ya pili..