Mwana wa Mfalme Salman kuandaa mbio

Mkuu wa chama kinachoongoza mbio za magari ya Langalanga yaani Formula 1 Bernie Ecclestone anasema kuwa amemwachia Mwana wa Mfalme wa Bahrain jukumu la kuandaa mbio za mwezi ujao zilizopangwa kufanyika Bahrain.

Image caption Uwanja wa Grand Prix Bahrain

Mbio hizo zikiwa ni za kufungua msimu wa mashindano ya mwaka huu zilikuwa mashakani kufuatia hali ya wasiwasi iliyotokea huko ambapo hadi sasa watu sita wanasemekana kuuawa katika ghasia za wananchi wanaotaka mageuzi.

Ecclestone ameiambia BBC kuwa Mwana wa Mfalme Salman bin Hamad al-Khalifah yuko katika nafasi bora ya kuamua kama mashindano hayo yanaweza kufanyika au la.

Ecclestonme ameongezea kuwa licha ya kumvisha jukumu hilo, wao hawatoruhusu watu kwenda nchini Bahrain ikiwa hali itaendelea bila kuwepo usalama.

Image caption Bw Bernie Ecclestone

Mwana wa Mfalme Salman ni mwanawe Mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa al Khalifah anayetarajiwa kumrithi babake. Kwa wakati huu ni yeye aliyekabidhiwa jukumu la kuongoza mazungumzo na makundi ya upinzani, ambayo yanasema kuwa hayatoanza mazungumzo hadi baadhi ya madai yao yakubalike.

Waandamanaji wameweka kambi ya maandamanao katika eneo lililo katikati mwa mji wa Manama baada ya vikosi vya usalama kuondolewa.

BBC Michezo inafahamu kwamba onyo la Bw.Ecclestone halitoshi kuanzisha vurumai ya makampuni ya bima kuziondolea timu za magari bima.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mwana wa Mfalme, Salma bin Hamad al-Khalifah

Endapo Bahrain itashindwa kuandaa mbio hizo kwenye tarehe iliyopangwa, Ecclestone amesema hadhani kama kuna nchi nyingine itakayokuwa tayari kuandaa mbio hizo kwa haraka.

Akaongezea kuwa mbio za Bahrain zitaahirishwa hadi tarehe tofauti ikiwa mbio za mwezi Machi zitashinda kuandaa.

Matamshi yake yanatokea kukiwa na habari kuwa baadhi ya Timu za magari zimetishia kususia endapo mashindano hayo yatafanyika.