Ancelotti asema hataondoka Chelsea

Meneja wa Chelsea Carlo Ancelotti, ameahidi kamwe hataondoka katika klabu hiyo baada ya mabingwa hao kutolewa katika patashika za kutetea kombe la FA.

Image caption Carlo Ancelotti

Kufungwa kwa mikwaju ya penalti siku ya Jumamosi na Everton kumewaacha Chelsea kuwa na matumaini pekee katika Ubingwa wa Ligi ya vilabu vya Ulaya msimu huu.

Alipoulizwa iwapo atafikiria kujiuzulu wakati huu wakisubiri kukabiliana na FC Copenhagen siku ya Jumanne, Ancelotti alisema: "Hapana, si mimi.

"Sipaswi kufikiria kazi yangu. Mwenye jukumu hilo ni mmiliki wa klabu, Roman Abramovich na si mimi."

Kufuatia kufungwa bao 1-0 na Wolves tarehe 5 mwezi wa Januari, Chelsea imeshinda mechi nne kati ya tano, lakini wameshindwa kufunga bao katika muda wa kawaida katika mechi tatu zilizopita, licha ya kumyakua mshambuliaji hatari Fernando Torres kwa paundi milioni 50.

Ancelotti amedai John Obi Mikel na Michael Essien hawapo katika kiwango chao kwa asilimia 100 na amekiri ni John Terry na Branislav Ivanovic pekee ndio wanaocheza kwa kiwango chao cha kawaida.

Kutetereka kwa Chelsea msimu huu wa Ligi Kuu ya England kunamaanisha kufuzu kwao kucheza Ligi ya Ubingwa wa Ulaya msimu ujao kupo mashakani.

Hali inayofanana na hii misimu miwili iliyopita ililazimisha kutimuliwa kwa meneja Luiz Felipe Scolari.

Lakini Ancelotti, ambaye katika msimu wake wa kwanza alifanikiwa kushinda ligi na Kombe la FA kwa mpigo, amesema kushinda katika mbio zao za kuwania Kombe la Ulaya kutafufua matumaini yote waliyonayo.