Gattuso afungiwa mechi nne

Kiungo wa AC Milan Gennaro Gattuso amefungiwa kucheza mechi nne baada ya kukabiliana na kocha msaidizi wa Tottenham Joe Jordan, katika mchezo wa ligi ya mabingwa Ulaya.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Gattuso akimkabili kocha wa Spurs, Jordan

Kiungo huyo alimpiga kichwa Jordan baada ya mchezo wa siku ya Jumanne kwenye uwanja wa San Siro.

Shirikisho la soka barani Ulaya limetoa adhabu hiyo baada ya mkutano wa nidhamu siku ya Jumatatu.

Gattuso, ambaye aliomba radhi kwa kosa hilo, ana siku tatu za kukata rufaa iwapo ataamua kufanya hivyo.

Hata kama rufaa hiyo itakubaliwa, hatoweza kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Tottenham, kwa sababu ana kadi ya manjano aliyoipata katika mchezo wa awali.

Mchezaji huyo kongwe wa Kiitaliano, alimpiga kichwa, baada ya kupatwa na hasira, kufuatia Tottenham kupata bao moja, katika mchezo wa timu 16, kwenye uwanja wa San Siro.