Blackpool yaisambaratisha Spurs 3-1

Blackpool iliisambaratishaTottenham katika kipindi pili na kwa urahisi wakwamua katika hofu ya eneo baya la kushuka daraja, na kuwasononesha Tottenham ambao wiki iliyopita waliopata ushindi mzuri dhidi ya AC Milan.

Charlie Adam alikuwa wa kwanza kufungua pazia la mabao kwa Blackpool baada ya mkwaju wa penalti baada ya mlinzi wa Spurs, Sebastien Bassong kumuangusha chini DJ Campbell.

Campbell akaongeza bao la pili kwa Blackpool baada ya kumalizia shambulio la kushtukiza kutokana na pasi ya pembeni ya James Beattie.

Bao la tatu la Blackpool liliwekwa kimiani na Ormerod katika dakika ya 80.

Spurs walipata bao la kufutia machozi lililofungwa na Roman Pavlyuchenko sekunde chache kabla ya mpira kumalizika.

Hata hivyo pamoja na kupoteza mchezo huo, Tottenham walikosa mabao mengi na sifa zimwendee mlinda mlango wa Blackpool, Kingson pamoja na walinzi wake kwa kazi nzuri ya kuokoa mabao ya wazi.

Ulikuwa usiku mzuri utakaokumbukwa na meneja wa Blackpool, Ian Holloway na timu yake, walioanza pambano hili wakiwa pointi mbili juu ya shimo la kuteremka daraja, lakini walipambana kufa na kupona na kuonesha kandanda safi na kujipatia ushindi mzuri.

Matokeo hayo yameipandisha Blackpool hadi nafasi ya 12 wakiwa na pointi 32.

Spurs wanaendelea kubakia nafasi ya nne na pointi 47.