Mapigano yachacha nje ya Tripoli

Wamajeruhi wafrika hospitali za Libya Haki miliki ya picha BBC World Service

Wanajeshi wanaomuunga mkono Kanali Muammar Gaddafi wametekeleza mashambulio katika miji iliyoko karibu na mji mkuu Tripoli, katika juhudi za kupanua maeneo wanayoyadhibiti.

Makabiliano makali yaliripotiwa magharibi mwa mji wa Zawiya ambapo walioshuhudia wamesema kuwa silaha nzito nzito zilitumika kuwashambulia waandamanaji ndani ya msikiti, na kuwaua takriban watu wasiopungua kumi.

Mashariki mwa mji kumetokea makabiliano makali kupigania udhibiti wa uwaja wa ndege ulioko karibu na mji wa Misurata.

Daktari mmoja ameiambia BBC kuwa hospitali yake imepokea majeruhi wapatoa 70.

Mkaazi mmoja anasema wanajeshi watiifu kwa Kanali Gaddafi wamefikuzwa kutoka mji huo.

Huku hayo yakiarifiwa, rais Barack Obama wa Marekani ametoa wito kwa viongozi wa Uingereza, Ufaransa na Italia washauriane juu ya hatua za kuchukua kukabili mzozo wa Libya.

Duru za awali kutoka Ikulu ya white house zilidokeza kuwa Obama anazingatia hatua kadhaa dhidi ya serikali ya Libya ikiwemo kuwekewa vikwazo.