Waandamanaji washambuliwa Tripoli

Waandamanaji wanaopinga serikali mjini Tripoli wameshambuliwa kwa nguvu kwa bunduki, kwa mujibu wa taarifa kutoka mji huyo mkuu wa Libya.

Haki miliki ya picha getty
Image caption Wandamanaji Tripoli

Maandamano mjini humo yalirejea wakati wanaotaka kumuondoa madarakani kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi walipotoka misikitini baada ya sala ya Ijumaa.

Kuna taarifa za vifo na watu kujeruhiwa, lakini hakuna taarifa zenye kuaminika kuhusu vifo hivyo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kanali Gaddafi akizungumza mjini Tripoli

Wakati huohuo, kituo cha televisheni cha taifa kimeonesha picha za Kanali Muammar Gaddafi akihutubia umati mkubwa katika eneo la wazi mjini Tripoli.

Alioneshwa akizungumza kutoka katika jengo moja la zamani, na kutoa wito kwa umati kubeba silaha na kutetea taifa, na mafuta yake dhidi ya waandamanaji wanaopinga serikali ambao wamedhibiti maeneo makubwa ya nchi hiyo.

"Hii ndio iliwateketeza Waitaliano," amesema, akikumbushia Libya ilivyowaondoa watawala wake wa kikoloni. "Mimi niko miongoni mwenu na tutapigana, na tutawashinda.

"Tutatokomeza ukandamizaji wowote kwa njia ya watu. Kwa kutumia watu wenye silaha, na itakapobidi tutafungua ghala letu la silaha, ili wananchi wote, na makabila yote ya Libya yawe na silaha. Libya itakuwa moto mkali, itakuwa mkaa unaoungua."

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waandamanaji mjini Benghazi

Wafuasi wake wamepeperusha bendera za kijani, ishara ya utawala wa Gaddafi. Amesema: "Maisha bila utu hayana maana, maisha bila bendera za kijani hayana maana. Imbeni, chezeni na mjiandae."

Baadaye, katika mkutano na waandishi wa habari katika Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, naibu balozi wa Libya katika umoja huo Ibrahim Dabbashi amemuelezea Kanali Gaddafi, ambaye amekaa madarakani kwa miaka 42, kama "mwendawazimu" na kuonya kuwa maelfu watakufa mjini Tripoli kwa sababu kiongozi huyo hatokimbia, na atapigana hadi mwisho.

Amewataka mabalozi wote wa Libya duniani kote kuukana utawala huo na kuweka wazi kuwa wanawakilisha wananchi na sio Kanali Gaddafi, na pia kuzitaka nchi za Afrika kutopeleka wanajeshi au misaada kwa serikali yake.