Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Mzee wa kifaru

Wanakijiji wa kijiji kimoja hapa Uingereza wamekasirishwa, baada ya mkazi mmoja wa kijiji hicho Nicholas Kravchenko kununua kifaru cha kijeshi.

Haki miliki ya picha wikipedia
Image caption Jamaa kapaki kama hiki mtaani kwake

Bwana huyo anayependa mambo ya kijeshi alitoa kiasi cha dola zaidi ya elfu ishirini kununua kifaru hicho cha kijani na kukiegesha nje ya nyumba yake. Taarifa za gazeti la Metro zimesema polisi waliitwa kwa haraka katika mtaa mtulivu huko Wolvercote, karibu na mji wa Oxford, na wenyeji wa huko kulalamika kuwa kifaru hicho kinawatisha.

Bwana Kravchenko, ambaye ni mhandisi mstaafu wa jeshi, alinunua kifaru hicho jeshini kwa ajili ya kujifurahisha na pia kukitumia kwa ajili ya shughuli za kuchagusha fedha za misaada.

Bwana huyo amegoma kabisa kukiondoa kifaru hicho mtaani kwake, ambacho huchukua nafasi ya magari matatu kukiegesha. Bwana Kravchenko anayejiita 'Mtu wa mizinga' amesema amechoshwa na chokochoko za majirani zake.

"Kama ningekuwa nimevunja sheria, baraza la kijiji na polisi wasingeniruhusu kufanya hivi" amesema mtu huyo wa mizinga.

Maafisa wa baraza la mji wa Oxford wanakutana kujadili jinsi ya kumshawishi bwana huyo kuondoa kifaru chake mtaani.

Wake 39, watoto 94, wajukuu 33

Bwana mmoja nchini India, mwenye wake thelatini na tisa, amesema hatojali sana iwapo atapata wake wengine wa kuwaoa. Bwana huyo, Ziona Chana, anaishi katika kijiji kimoja cha mbali, kaskazinimashariki mwa India, pia ana watoto tisini na wanne, na wajukuu thelathini na watatu.

Haki miliki ya picha amazing facts
Image caption Bwana Chana akiwa na familia yake

Shirika la habari la Reuters limesema wote hao wanaishi katika nyumba moja yenye vyumba mia moja, katika kijiji cha milimani kwenye jimbo la Mizoram, karibu na mpaka na Myanmar na Bangladesh.

"Kuna wakati nilioa wake kumi katika kipindi cha mwaka mmoja" amekaririwa bwana huyo akisema.

Wake zake wanaishi pamoja katika bweni moja kubwa karibu na chumba cha bwana Ziona, na wenyeji wa huko wanasema hupendelea kuwa na wake zake saba au nane kila wakati.

Watoto wake wakubwa wa kiume, na watoto wao huishi katika vyumba tofauti, katika jengo hilo hilo.

Hata hivyo familia hiyo, hutumia jiko moja.

Wake hao huwa na zamu ya kupika, wakati watoto wa kike shughuli zao ni kusafisha nyumba na kufua.

Haki miliki ya picha amazing facts
Image caption Nyumba ya Chana yenye vyumba 100

Watoto wa kiume hufanya vibarua kama vile ukulima na kuchunga mifugo.

Familia hiyo ambao kwa jumla wapo 167, hula kilo 91 za mchele na 59 za viazi kila siku.

"Hata leo niko tayari kuongeza familia yangu kwa kuoa mke mwingine" amesema Ziona. Bwana Ziona alikutana na mke wake wa kwanza wakati akiwa na miaka kumi na saba. Mke wake huyo amemzidi kwa miaka mitatu.

Digrii zinalipa

Image caption Mambo ya digrii

Nchini Uchina vijana makapera, yaani ambao hawajaoa wanatafuta wake wenye shahada za juu za chuo kikuu, yaani degree kwa sababu kuna faida za kifedha.

Wanaume katika jimbo la Guangdong, ambao wameoa wanawake wenye degree, hupatiwa yuan 3,000, sawa na dola 362.

Mtu mwingine wa hivi karibuni aliyezawadiwa, amepewa dola 181 kwa kuoa mwanamke mwenye diploma.

Mtandao wa chinadaily.com umesema mamlaka za kijiji hicho zinasema, sera hiyo inasaidia kukuza idadi ya watu katika eneo hilo, ambalo limeendelea kimaisha, lakini kimawazo na kielimu liko nyuma.

Mwizi wa msumeno

Bwana mmoja nchini Marekani aliiba msumeno wa umeme na kuuficha ndani ya suruali yake, katika duka moja la vifaa vya ujenzi.

Mtandao wa Cnews.com umesema tukio hilo limetokea mjini Oklahoma.

Wafanyakazi wa hilo lijulikanalo kama Chikasha, walishangaa kuona mteja akitembea kwa mtindo wa aina yake, na mwanzo wakidhani labda ni mlemavu.

Hata hivyo walikuwa wakijiuluza kwa nini suruali yake imetuna sana sehemu za kati.

Wafanyakazi hao wamesema bwana huyo alikuwa akienda mwendo wa taratibu akielekea kutoka nje ya duka. Hata hivyo, wafanyakazi wa dukani walimshtukia kwamba anafanya jambo la kihalifu, na alivyoona anaanza kufuatwa, aliutoa msumeno huo, na kukimbia.

Polisi walimkamata mwizi huyo aliyekimbia na kupanda juu ya mti.

Bia kuwa pombe

Hatimaye bia imetambuliwa rasmi kuwa ni pombe nchini Urusi.

Hii ni moja ya Hatua kali za kupambana na ulevi nchini humo tangu kuanguka kwa umoja wa kisovieti. Bia hutambulika kama chakula na huuzwa muda wote mitaani.

Image caption Bia kutazamwa tofauti

Muswada wa kubadili mtazamowa kinywaji hicho umewasilishwa bingeni wiki hii. "Hatua hiyo ni muhimu sana na itasaidia kukuza afya za wananchi wetu" amesema Yevgeny Bryun akikaririwa na gazeti la Telegraph.

Ikipita sheria hiyo, itapiga marufuku uuzaji wa bia usiku, na katika maeneo mengi ya wazi ikiwa ni pamoja na karibu na shule, na kupunguza ukubwa wa kopo za bia.

Ingawa Vodka inaendelea kuwa kinywaji maarufu nchini humo, unwaji wa bia umeongezeka kwa zaidi ya mara tatu katika miaka kumi na tano iliyopita, kutokana na kuuzwa kwa bei ya chini, upatikanaji wake kirahisi na kutokuwepo kwa usimamizi, na pia kutazamwa kama ni chakula, badala ya pombe.

Na kwa taarifa yako...Ulaya ndio bara pekee duniani lisilokuwa na jangwa....

Tukutane wiki ijayo....Panapo majaaliwa

Taarifa kutoka mitandao mbalimbali duniani