Maelfu waendelea kukimbia machafuko Libya

Raia wa kigeni wakivuka mpaka wa Tunisia Haki miliki ya picha BBC World Service

Juhudi za kimataifa zinaendelezwa huku maelfu ya watu wakiendelea kwenda kwenye mpaka wa Libya na Tunisia,kukimbia machafuko Libya.Zaidi ya wakimbizi elfu thelathini wengi wao wakiwa raia wa Misri wamekwama.Mwandishi wa BBC anasema hiyo jana zaidi ya watu ellfu kumi na mbili walivuka mpaka.

Katika muda wa wiki moja iliopita watu zaidi ya elfu hamsini wamekimbilia katika eneo la mpaka huo na hakuna dalili kwamba hali hiyo itapungua,wengi wao wakiwa wafanyakazi wa kawaida, raia wa Misri na wanatafuta njia ya kurudi nyumbani.Baadhi yao walipata msaada wa mikate na maji kutoka kwa raia wa Tunisia waliojitolea kuwasaidia.

Huku wengine wakikimbilia kwenye mipaka, mamia ya raia wa kusini mwa jangwa la sahara ni miongoni mwa maelfu ya watu waliopewa msaada wa kutoka nje ya Libya. Raia karibu 500 wa Nigeria waliokuwa Libya waliwasili mjini Abuja jana.

Kwa Gaddafi na familia yake mambo yanazidi kuwa magumu serikali ya Uingereza imezuia mali za Gaddafi nchini humo pamoja na jamii yake na waakilishi wao.Haijulikani thamani yake lakini inasemekana kuwa mamia ya mamilioni ya madola.Hatua hii inafwatia uamuzi wa baraza la usalama la umoja wa mataifa siku ya jumamosi . Marekani na Uswizi pia tayari wametangaza kusitisha shughuli za biashara kwa makampuni yanayohusiana na kiongozi huyo wa Libya.

Mmoja wa watoto wa kiongozi wa Libya Muammar Gadaffi ameelezea wasiwasi wake kuhusu uamuzi wa umoja wa mataifa kuwekea jamii ya Gaddafi vikwazo vya kusafiri nje ya nchi.Saadi Gadaffi,aliyekuwa mchezaji mpira wa miguu wa kulipwa na mwanawe Gaddafi wa tatu,amesema maisha yake yote amekuwa akisafiri sana nje ya nchi na sasa itamlazimu atafute huduma za wakili ili aendelee kufanya hivyo.

Katika mahojiano na BBC alieleza hali ilivyo sasa kama tetemeko la ardhi;homa itakayoeneza machafuko na akasema kwamba kama babake ataondoka Libya,nchi hiyo itazama katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe saa moja baada ya babake kuondoka.