Waziri mkuu wa Tunisia ajiuzulu

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Tunisia

Waziri mkuu wa Tunisia Mohammed Ghannouchi ametangaza kupitia televisheni ya taifa kuwa anajiuzulu- matakwa muhimu kutoka kwa waandamanaji.

Alikuwa akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Tunis, baada ya kutoa hotuba ndefu akijitetea wakati alipokuwa madarakani.

Bw Ghannouchi anaonekana kuwa karibu sana na aliyekuwa Rais Zine al-Abidine Ben Ali, aliyeondoshwa madarakani mwezi uliopita.

Bw Ghannouchi, mwenye umri wa miaka 69, amekuwa chini ya uongozi wa Bw Ben Ali tangu mwaka 1989.

Alisema, " Baada ya kutafakari kwa zaidi ya wiki moja, nikaanza kushawishika, na familia yangu iliniunga mkono, na hivyo kuamua kujiuzulu. Si kwamba nakimbia majukumu yangu; nimekuwa nikitimiza wajibu wangu tangu Januari 14."

Aliongeza, " Siko tayari kuwa mtu anayechukua uamuzi utakaoishia kusababisha vifo."

"Kujiuzulu huku kutasaidia Tunisa, mapinduzi pamoja na maendeleo ya siku za usoni za Tunisia." Alisema.

Baada ya saa kadhaa mbadala wa Bw Ghannouchi alitajwa- Beji Caid Essebsi, mwenye umri wa miaka 84, ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje katika serikali ya marehemu Rais Habib Bourguiba.

Awali, polisi mjini Tunis walirusha mabomu ya kutoa machozi na risasi za onyo kutawanya maandamano ya hivi karibuni wakitoa wito wa kutaka serikali mpya na katiba mpya katika siku ya tatu ya ghasia.