Carling Cup: Wenger asita kulaumu

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amesita kuwalaumu wachezaji wake baada ya kufungwa 2-1 na Birmingham na kukosa kunyakua Kombe la Carling.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Arsene Wenger

Kuchanganyana kati ya mlinda mlango Wojciech Szczesny na mlinzi Laurent Koscielny, kulimuwezesha Obafemi Martins kuutumbukiza mpira katika nyavu tupu dakika ya 89.

"Kutolewana huko kidogo kumekuwa na athari kubwa katika mchezo na wachezaji wote wawili wamefadhaishwa sana. Simlaumu yeyote," Wenger aliiambia BBC.

"Wakati mambo yakiharibika dakika za mwisho katika mchezo, kunakuwa hakuna muda wa kurekebisha."

Arsenal haijashinda kikombe tangu ilipoilaza Manchester United kwa mikwaju ya penalti kwenye fainali ya Kombe la FA mwaka 2005.

Wenger amekiri kushindwa kuchukua kombe safari hii, ni "jambo gumu sana kulikubali". Meneja huyo wa the Gunners ameongeza: "Wachezaji wamevunjika moyo, lakini hatuna budi kujizoazoa na hivyo ndivyo timu inatakiwa iwe. Ni nafasi nzuri kuonesha uimara wetu kifikra, jambo ambalo naamini ni muhimu.

"Tumepata kile tulichotarajia kutoka kwa Birmingham. Ni timu inayopigana kiume na kusababisha matatizo mengi makubwa kwa mipira ya mbali.

"Nawapongeza, wamepata kombe, lakini tunasikitika namna tulivyofungwa bao la pili."

Kukataa kwa Wenger kusajili mlinda mlango na mlinzi imara wa kati, kwa mara nyingine kumezua gumzo kufuatia makosa ya mlinzi aliyesajiliwa msimu huu Koscielny, na mlinda mlango Szczesny.