Bowyer kuondoka Birmingham msimu ujao

Kiungo wa Birmingham, Lee Bowyer hatarajii kupatiwa mkataba mpya wakati mkataba wake wa sasa utakapomalizika baadae mwaka huu.

Image caption Lee Bowyer

Bowyer, mwenye umri wa miaka 34, alikuwemo katika kikosi kilichochukua Kombe la Carling dhidi ya Arsenal, lakini amethibitisha kwa sasa anatafuta klabu nyingine mpya.

Alipoulizwa iwapo ataongezewa mkataba mpya, alisema: "Nadhani kwa sasa klabu imesema "hapana".

"Hilo kamwe halo halitawezekana, kwa hiyo nafuta sehemu kwengine. Labda wanaweza kubadili mawazo na kunibakisha, huwezi kujua. Lakini hilo ni jukumu la klabu yenyewe."

Bowyer amesisitiza anapenda kuendelea kubakia St Andrews pamoja na matokeo mazuri dhidi ya Arsenal lakini amekiri: "Suala hilo sina uwezo nalo. Ninachoweza kufanya ni kucheza soka yangu vizuri zaidi."

Mchezaji huyo aliyezaliwa London na kujiunga na Birmingham mwaka 2009 akitokea West Ham, anaamini bado kiwango chake kinamuwezesha kuchezea klabu kubwa.

"Kwa sababu ya umri, watu bado wanahoji iwapo unaweza kucheza kwa kiwango cha juu, iwapo utaweza kufanya hivyo vitu ulivyokuwa ukifanya siku za nyuma. Lakini nadhani nilionesha kiwango cha juu dhidi ya Arsenal.

"Nimeshafunga mabao muhimu msimu huu, dhidi ya Chelsea, Manchester United na katika nusu fainali dhidi ya West Ham. Pia ninayo rekodi nzuri barani Ulaya, nimepachika mabao machache kwenye mashindano ya Ulaya."

Iwapo Bowyer ataondoka, basi hata hivyo atakuwa amefanikiwa kupata medali yake ya kwanza katika muda wake mrefu wa usakataji soka.