Boti jipya la wahamiaji lawasili Italia

Boti moja lililokuwa limebeba wahamiaji haramu 347 kutoka Tunisia limewasilia Italia, na kusababisha wasiwasi wa uhamiaji upya wa kuvuka upande huo baada ya wiki moja wa kuwepo hali mbaya ya hewa.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wahamiaji Lampedusa

Boti hiyo ya uvuvi iliwapeleka wahamiaji katika kisiwa kidogo cha Lampedusa, takriban kilomita 100 kupitia bahari ya Mediterranean kutoka pwani ya Tunisia.

Maelfu ya watu wamewasili kisiwani hapo tangu mwezi Februari, kufuatia ghasia za nchini Tunisia.

Waziri wa mambo ya ndani wa Italia, Roberto Maroni, alisema kuna hofu ya kupokea wahamiaji haramu kutoka Libya pia.

Alisema, kuna wahamiaji haramu milioni 1.5 ndani ya Libya.

" Sasa wanakimbilia upande wa magharibi {Tunisia} na mashariki {Misri} lakini siku za usoni wanaweza pia kuelekea kaskazini {wakielekea Italia}." Aliliambia bunge.

Bw Maroni, mwanachama wa jumuiya ya kupinga uhamiaji wa kaskazini, alionya juu ya "dharura ya kibinadamu" alipokutana na mawaziri wa mambo ya ndani wenziwe kutoka Umoja wa Ulaya mjini Brussels wiki iliyopita.

Maafisa wengine wa umoja huo walisema Roma imehamaki kutokana na mgogoro uliopo Mediterranean.