Wasi wasi wa ghasia wazidi Sudan Kusini

Wakati raia wa Sudan walipokuwa wakipiga kura ya maoni kuamua endapo wanataka kujitenga au la, wito wao ulikuwa hiyo ni fursa ya kutumia visanduku vya kura na siyo risasi.

Lakini milio ya risasi bado inatawala anga za Sudan Kusini huku kukiwa na uasi uliozuka katika jimbo la Jonglei ulioanzishwa na mpiganaji wa zamani wa Jeshi la kusini, Jenerali George Athor aliyejitenga kutoka chama cha SPLM mwaka jana.

Yeye alitaka kuwa Gavana wa jimbo hilo, lakini chama cha SPLM kikampuuza, na alipojaribu kusimama kama mgombea huru akashindwa.

Tangu hapo amekuwa akipigana na vikosi vya Sudan Kusini. Kupitia kipindi kirefu cha vita vya wenyewe nchini Sudan upande wa kaskazini ulitumia ujanja wa kugawanya katika kupambana na sehemu ya kusini.

Kutokuaminiana

Kuna dhana miongoni mwa wakuu wa SPLM kwamba huenda George Athor anatumiwa na kupokea msaada kutoka utawala wa kaskazini.

Hali kama hiyo imezua wasiwasi katika eneo la Abyei lenye utajiri wa mafuta na ardhi yenye rutuba baina ya makabila ya huko, wa Misseriya wenye uhusiano na wakuu wa Khartoum na wa Dinka wa kusini.

Msemaji wa jeshi la kusini, Philip Aguer, ameielezea sehemu hiyo kama inayokabiliwa na hatari. Ameiambia BBC kuwa mgambo wa kaskazini wakiwa na silaha kali wamewazidia polisi, na kuchoma vijiji na maeneo yaliyo karibu na Abyei. Mapambano haya katika sehemu mbili tofauti bila shaka yanapunguza matumaini ya raia.

Wote wanasubiri uhuru lakini amani bado inawakwepa.