Wanawake I Coast 'wafyatuliwa risasi'

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu wakionyesha damu ya wanawake wanaodaiwa kupigwa risasi na majeshi ya serikali

Walioshuhudia walisema, majeshi ya usalama Ivory Coast yamewapiga risasi takriban wanawake sita waliokuwa wakiandamana wakimwuunga mkono Alassane Ouattara katika mji mkuu wa Abidjan.

Bw Ouattara anatambulika na Umoja wa Mataifa kama mshindi wa uchaguzi wa mwezi Novemba, lakini Laurent Gbagbo amekataa kuachia madaraka.

Ufyatuliaji huo wa risasi umetokea Abobo, eneo linalomwuunga mkono Ouattara kwa kiwango kikubwa ambalo limekuwa na vurugu kwa zaidi ya wiki moja.

Ghasia za hivi karibuni zimeushinikiza umoja huo kutoa onyo la kuwepo wasiwasi wa kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Idrissa Diarrassouba, mkazi wa Abobo ameliambia shirika la habari la Reuters, " Watu wenye kuvaa sare wamekuja na magari yao na kuanza kufyatua risasi kiholela."

Wanawake hao ni wanachama wa muungano wa chama cha kisiasa cha Ouattara, RHDP.

Umoja wa Mataifa umesema takriban watu 200,000 wamekimbia wilaya ya Abobo katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita.