Mahakama yachunguza 'uhalifu'wa Gaddafi

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Brega

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu amesema atamchunguza kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, watoto wake wa kiume na viongozi waandamizi kwa uhalifu dhidi ya binadamu.

Luis Moreno-Ocampo alisema hakuna mwenye haki ya kuwaua raia.

Maelfu ya watu wanadhaniwa kufariki dunia katika ghasia baada majeshi ya usalama kuwalenga waandamanaji katika vurugu zilizoanza Februari 17.

Kanali Gaddafi aliahidi kuendelea kupambana licha ya kukosa udhibiti wa eneo kubwa la nchi hiyo.

Vyanzo vya habari mjini Brega vilisema, mapema siku ya Jumatano majeshi yake yalishambulia kwa kutumia ndege katika mji huo wenye mafuta.

Mashambulio hayo yalifanyika siku moja baada ya kuwepo mapigano baina ya waasi na majeshi ya serikali katika mji ambapo watu 14 walifariki dunia.

Alisema, " Ofisi ya mwendesha mashtaka aliamua kufanya uchunguzi kwa madai ya uhalifu dhidi ya binadamu yaliyofanywa Libya tangu Februari 15."

" Ujumbe wa waandamanaji waliofanya kwa amani walishambuliwa na majeshi ya usalama.

" Katika wiki zijazo ofisi hii itachunguza ni wepi wanahusika zaidi katika mashambulio mazito zaidi, na kwa uhalifu mbaya zaidi uliofanywa Libya."

Lakini mwendesha mashtaka huyo pia alisema upinzani nao utachunguzwa kama ulifanya uhalifu wowote.