Ivory Coast yakumbwa na tisho la vita

Tukio la shambulio dhidi ya wanamama Haki miliki ya picha BBC World Service

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeezea hofu ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory Coast, na kuamrisha walinda amani wake kutumia njiya zote ili kuwalinda raia.

Hapo Alhamisi wanajeshi watiifu kwa Laurent Gbagbo anayeng'ang'ania madaraka licha ya kushindwa kwenye uchaguzi Mkuu waliwafuatilia risasi wanawake waliokuwa wakiandamana mjini Abdijan kumuunga mkono Alassane Ouattara anayetambuliwa kushinda uchaguzi huo kimataifa.

Takriban wanawake sita waliuawa kwenye tukio hilo.Wakati huo huo mshirika wa karibu wa Bw. Ouattara ameitaka jamii ya kimataifa kuchukulia mzozo wa kisiasa nchini Ivory Coast kwa uzito sambamba na hali ilivyo huko Libya.

Mwakilishi wa Kambi ya Ouattara katika Umoja wa Mataifa Youssoufou Bamba amesema wapinzani wao wanatumia silaha za vita kuwalenga raia wasio na hatia.